Na Hadija Bagasha Tabora,
MGOMBEA urais wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema iwapo atapata ridhaa ya kuwaongoza Watanzania atahakikisha anafufua viwanda vya kuzalisha nyuzi na nguo nchini ili zao la pamba lilimwe kwa wingi na wakulima waweze kunufaika.
Mgombea urais huyo ametoa ahadi hiyo wakati wa mikutano yake ya kampeni mkoani Tabora jana. Aliahidi kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wakulima na wafugaji.
Awali akihutubia wananchi wa Igunga katika viwanja vya Sokoine, mkoani Tabora Profesa Lipumba alisema Serikali ya CCM imeahidi wananchi kuwa itafufua viwanda kitendo ambacho hakijatekelezeka ndani ya miaka mitano
Profesa Lipumba amesema endapo chama hicho kitapata ridhaa ya uongozi kutoka kwa wananchi atahakikisha anafufua viwanda vya nguo na nyuzi ili wakulima wa pamba waweze kunufaika.
Amesema ili kukuza viwanda ni lazima kuendeleza kilimo chenye tija kitakachowanufaisha wakulima pamoja na kuwekeza kwenye kilimo na kufufua viwanda.
“Ndugu zangu nilipopita Mkoa wa Morogoro wiki iliyopita, kiwanda cha nguo kimekufa lakini palikuwa na viwanda vingi Dar es Salaam, navyo havifanyi kazi ili kumnufaisha mkulima wa pamba. Ni lazima pawe na soko,” amefafanua Profesa Lipumba.
Mgombea huyo pia amegusia kilimo cha mpunga na ufugaji wa ng’ombe wa kisasa, ambapo aliwaahidi wananchi wa Igunga kuwa endapo atapata ridhaa atahakikisha anafufua kiwanda cha ngozi ili wafugaji waweze kunufaika.
“Kiukweli ngozi ina faida nyingi endapo kutakuwa na kiwanda, kitawasaidia utengenezaji mikanda, viatu na mapambo mbalimbali ili kuongeza kipato na ajira,” amesema.
Awali akizungumza na waandishi wa habari jana, Profesa Lipumba alisema lengo la chama hicho kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa endapo kitapata ridahaa.
Alisema dhumuni kubwa ni kupata Katiba mpya itakayoshirikisha vyama vyote na wasio na vyama ili kudumisha misingi ya demokrasia.
“Tukizungumzia kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa ni pamoja na kuleta haki sawa kwa kwa pande zote mbili na kupata Tume huru ya uchaguzi,” amefafanu Profesa Lipumba.
Sambamba na hayo, alisema Tume ya Jaji Warioba ilifanya kazi kubwa ya kukusanya maoni ya wananchi lakini haikufanikiwa kukamilika kwa kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano suala la Katiba halikuzungumzwa kabisa.
“Chama Cha Wananchi CUF ndani ya miezi mitatu ya mwanzo lazima tuandae utaratibu wakupata katiba mpya itakayoshirikisha wananchi na kuleta usawa kwa pande zote mbili,” alisema
Aidha Profesa Lipumba amefafanua umuhimu wa kuwa na utawala wa sheria, ambapo alisema zipo kesi nyingi ambazo watu wako ndani lakini hawajapata haki.
Kutokana na alichodai ukiukwaji huo, alisema ipo haja ya kuwa na utawala unaoheshimu sheria na kujali haki za msingi za mwananchi mmoja mmoja.
“CUF tutakapoingia madarakani tutaunda chombo kitakachoweza kuajiri majaji na mahakimu ili kuwezesha mahakamani zote ziweze kutenda haki kwa mujibu wa sheria,” alisema
Akiomba kura mgombea ubunge wa Jimbo la Igunga, Frank Masunga alisema endapo atachaguliwa atahakikisha anashughulikia suala la ajira kwa vijana.
Amesema tangu mwaka 2015 tatizo la ajira limekuwa changoto kutokana na fedha kukaliwa na watu wachache na kusababisha watu kushindwa kupata fedha kwa ajili ya mitaji.
“Wapo wanafunzi waliomaliza vyuo, lakini hawana ajira kazi imekuwa kushinda vijiweni,ndugu zangu mkinipa fursa nitahakikisha suala la ajira kwa vijana waliomaliza elimu ya juu nalishughulikia,” amesema Masunga
Suala lingine aliloahidi kushughulikia ni pamoja na haki za binadamu, akidai kumekuwepo na kesi nyingi zinazopelekwa mahakamani, lakini hazitolewi uamuzi kwa wakati.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime