Na Wizara ya Kilimo
Serikali imeanza kuchukua hatua za haraka kuumaliza mgogoro wa eneo lililo ndani ya Taasisi ya utafiti wa Kilimo (TARI UYOLE) lililopo kata ya Ilomba mkoani Mbeya.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana Tarehe 9 Aprili 2020 ametangaza hatua za serikali katika kutatua mgogoro huo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Mbeya akiwa ameambatana na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Albert Chalamila na kulikagua eneo hilo na kuzungumza na wananchi husika.
Waziri Hasunga ameiagiza Taasisi ya TARI Uyole kutoendelea na shughuli za utafiti mpaka hapo kesi ya mgogoro huo iliyopo mahakamani itakapotolewa uamuzi.
Kwa upande wa wananchi, Waziri Hasunga amewataka kusitisha shughuli zote za kilimo ili kusubiri maamuzi ya mahakama. Kuhusu mazao ambayo yalishalimwa na wananchi hao amesema kuwa wataruhusiwa kuvuna lakini hawataruhusiwa kuendelea na kilimo.
Wananchi hao wapatao 200 kwa mujibu wa orodha waliyoiandika na kusaini kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko yao kwa katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo Januari 1, 2020 wanailalamikia serikali kwa kutowalipa fidia kwa wakati hivyo kuiomba kuwalipa fidia ama kuwarudishia eneo hilo.
Eneo hilo lenye ukubwa wa Hekta 8.52 limekuwa likitumiwa na wananchi hao kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja na ufugaji.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila amewasihi wananchi hao kadhalika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Uyole kuitikia maelekezo ya Waziri wa Kilimo kwani serikali itafanya maamuzi ya busara na kila mtu atapata haki yake inayostahili.
Na endapo mahakama itabaini kuwa wanastahili kurudishwa eneo hilo watapatiwa kwa mujibu wa sheria na kama itabaini hawana haki kadhalika itafanya maamuzi.
More Stories
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza