Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) imesisitiza kuwa mafanikio ya taasisi za kifedha zinazomilikiwa na Serikali yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia matokeo ya huduma zake katika maisha ya wananchi, badala ya kuangalia idadi ya mikopo inayotolewa au kiasi cha fedha kinachowekezwa pekee.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa OTR, Sabato Kosuri, amesema hayo Oktoba 28, 2026, jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Msajili wa Hazina katika kikao kazi kati ya Mfuko wa SELF (Self Microfinance Fund), wahariri na waandishi wa habari, kilichoratibiwa na ofisi hiyo.
Kosuri amesema taasisi za kifedha zinazomilikiwa na Serikali zina jukumu muhimu katika kukuza uchumi jumuishi kwa kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wa makundi mbalimbali na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi zinazoongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Amesema Mfuko wa SELF una nafasi muhimu katika kuwawezesha wajasiriamali, wakulima na wanaotekeleza shughuli zinazohusiana na uhifadhi wa mazingira, hivyo mafanikio yake yanapaswa kutathminiwa kwa kuzingatia mchango wake katika maendeleo ya jamii.
Amefafanua kuwa tathmini ya mfuko huo haipaswi kuishia katika idadi ya mikopo inayotolewa au thamani ya fedha hizo, bali inapaswa kuangalia matokeo yanayopatikana kwa wanufaika, wakiwemo wanawake na vijana ambao ni makundi muhimu katika maendeleo ya taifa.
“Tunapozungumzia taasisi ya fedha kama Mfuko wa SELF, tunapaswa kuangalia athari na matokeo ya huduma zake katika jamii, badala ya kuzingatia idadi ya mikopo na kiasi cha fedha kinachotolewa pekee,” amesema Kosuri.

Amesisitiza kuwa kuangalia matokeo ya huduma za kifedha ni muhimu katika kubaini namna taasisi hizo zinavyosaidia wananchi kukuza shughuli zao za kiuchumi, kuongeza kipato na kuboresha maisha yao, hususan kwa makundi yenye uhitaji wa fursa za kifedha.


More Stories
NeST yafungua milango ya uchumi kwa vijana,wanawake
TFC yaongeza tija ya kilimo kupitia mbolea sahihi
JKCI, HTAF kukusanya bil. 25 kutibu watoto wenye magonjwa ya moyo