March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodaboda,wavuvi Ilemela wahamasishwa kusikiliza na kuchagua viongozi kwa amani

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Maofisa usafirishaji pamoja na wavuvi wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza, wamehimizwa  kujitokeza katika mikutano ya kampeni ili kusikiliza sera za wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa.

Hatua itakayowasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi bora kwa ustawi wa shughuli zao na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela Herbert Bilia, akizungumza katika kikao cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa viongozi wa maofisa usafirishaji ikiwemo bodaboda, bajaji, daladala pamoja na viongozi wa BMU(wavuvi

Akizungumza Septemba 11,2025 katika kikao cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa viongozi wa maofisa usafirishaji ikiwemo bodaboda,bajaji,daladala pamoja na viongozi  wa BMU(vikundi vya uvuvi), Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela, Herbert Bilia,amesisitiza umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani,utulivu na kufuata sheria bila kukubali kutumika kuvuruga amani.

“Tuungane kuwasikiliza wagombea wetu katika kampeni,tusikilize sera zao kwa sababu ni haki yetu ya msingi.Lakini tusikubali kutumika kuvuruga amani kwani mchakato wa wagombea kuchukua fomu na kurudisha ulifuata kanuni na taratibu za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,”amesema Bilia.

Bilia amesema,Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),inatamani kuona uchaguzi wa mwaka huu unafanyika kwa amani na mshikamano kwa kuwa maisha huendelea baada ya uchaguzi.

“Mshiriki uchaguzi vizuri katika misingi ya amani,utulivu na mshikamano, uchaguzi unapita lakini maisha yetu lazima yaendelee.Hatupaswi uchaguzi utuache tukiwa tumetengana,”amesema Bilia.

Kwa upande wake Ofisa Uchaguzi wa Jimbo la Ilemela,Shilinde Malyagili, amesema,sekta hiyo ya  usafirishaji  kupitia bodaboda ni moja ya sekta ambazo siyo rasmi lakini imeajiri  watu wengi  na nguzo ya uchumi wa nchi.

 Hivyo wameona ni  muhimu kuwapatia viongozi  wa makundi hayo elimu ya mpiga kura ili wakawahamasishe wananchama wao,Oktoba 29,2025 kujitokeza kupiga kura na kuchagua kiongozi sahihi atakaye waletea maendeleo  kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Naye Katibu wa Bodaboda Kata ya  Shibula,Abdullahshid Hussein,amesema,kama bodaboda wanapaswa kutumika kutunza amani ya nchi pamoja na kuhimiza wananchama wao kuhudhuria kwenye kampeni mbalimbali za wagombea na kufanya chaguo sahihi la viongozi.

Baadhi ya washiriki wa kikao cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa viongozi wa maofisa usafirishaji ikiwemo bodaboda, bajaji, daladala pamoja na viongozi wa BMU(wavuvi

Hussein amesema,baada ua uchaguzi maisha yanaendelea hivyo amewasihi bodaboda  wenzake kutotumika  vibaya kwani ikitokea vurugu wanaweza  kupigiwa au kupata matatizo na kukaa ndani huku mgombea anaendelea  na maisha yake.

“Wadau wote tunaofanya usafirishaji tuwe watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi ili uishe  salama na tuendelee na maisha yetu tukiwa salama,”amesema Hussein.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Maofisa Usafirishaji mtaa wa Kabambo Kata ya Kiseke jimboni Ilemela,Pendo Francis,amewahimiza wanawake wenzake kuwaunga mkono wagombea wanawake ili waweze kuleta maendeleo kwani uwezo huo wanao.