Na Bakari Lulela,Timesmajira
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, leo amefanya kampeni za kipekee katika Wilaya ya Handeni, akipita kata kwa kata kama ishara ya kuenzi wilaya yake ya asili na kushirikiana na wananchi wa nyumbani kwao.
Katika ziara hiyo ya kampeni, Doyo alitembelea kata ya Michungwani, Kabuku na Mkata, ambako alizungumza na wananchi na kusikiliza changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku.
Akiwa Michungwani,. Doyo aliwaeleza wananchi sababu kuu zinazochangia mazao ya wakulima wa Handeni kukosa thamani ya soko. Alisema kuwa miundombinu duni na ukosefu wa masoko ya uhakika vimekuwa kikwazo kikubwa, hali inayowapa nafasi madalali kuwanyonya wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei ya chini.
Ameeleza kuwa takribani asilimia 33 ya barabara za vijijini hazipitiki mwaka mzima kwa wakati kutokana na ukosefu wa barabara zenye kiwango kizuri, mifereji ya kupitisha maji na madaraja imara. Hali hii imesababisha wakulima kushindwa kusafirisha mazao na bidhaa zao kwa wakati, hivyo kusababisha kuporomoka kwa kipato na kuongeza umasikini vijijini, hususan katika wilaya ya Handeni.
Doyo ameahidi kuwa, endapo wananchi wa Handeni watamchagua kuwa Rais, atalipa hadhi zao la machungwa kwa kulifanya kuwa zao la kimataifa. Aidha, ameahidi kujenga kiwanda cha kusindika machungwa ili wananchi wa maeneo hayo wapate ajira na kipato cha uhakika.
“ Tafiti zinaonyesha zao la chungwa kutoka Handeni na Tanga kwa ujumla lina ubora kuliko chungwa lolote kutoka ukanda wa Afrika Mashariki. Haiwezekani wananchi wa Handeni wasifaidi tunu huyo, ilhali machungwa yao yana thamani kubwa kimataifa. Mkiniamini, tutajenga kiwanda hapa hapa Handeni,” alisisitiza Doyo.
Akiwa Kabuku, Doyo aligusia pia sera ya afya inayopatikana katika ilani ya Chama cha NLD. Amewaeleza wananchi kuwa serikali yake itahakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa gharama nafuu kupitia bima ya afya ya lazima na yenye upatikanaji rahisi kwa kila mwananchi. Aidha, alisisitiza kuwa huduma kwa mama wajawazito zitakuwa bure, hatua itakayowapa heshima wanawake wa nchi hii na kulinda maisha ya mama na mtoto.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampeni wa mgombea huyo, Pogora Ibrahim Pogora, alisema ni wajibu wa wananchi wa Handeni kumchagua Doyo kwa wingi wa kura. “Ni aibu kubwa kwa watu wa Handeni wasipompigia kura Mhe. Doyo, wakati wenzao wa Pwani
wameshajipanga kumpa kura. Doyo ni mtoto wenu, mnapaswa kumthamini na kumuunga mkono ili kesho aweze kutatua kero zenu, zikiwemo changamoto za maji ambazo zimekuwa tatizo kubwa Handeni,” alisema Pogora.
Msafara wa mgombea huyo unaendelea na kampeni, kuelekea, Kilindi, Kiteto na hatimaye Manyara, ambako mgombea huyo ataendelea kuwasilisha sera na dira yake kwa wananchi katika kampeni zake.

More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro