Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar
BARAZA la Mtihani la Taifa Tanzania (NECTA) limesema kuwa jumla ya wanafunzi 1,172,279 wa darasa la saba kutoka shule 19,441 za Tanzania Bara wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) kwa mwaka 2025, kuanzia Septemba 10 hadi 11 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam Septemba 9,2025 Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Ally Mohamed,amesema kati ya watahiniwa hao, 1,172,279 waliosajiliwa wavulana ni 535,138 sawa na asilimia 45.65 na wasichana ni 637,141 sawa na asilimia 54.35
“Kati ya watahiniwa hao, 1,094,321 sawa na asilimia 93.35 watafanya mtihani kwa Kiswahili, huku 77,958 sawa na asilimia 6.65 wakifanya mtihani kwa Kiingereza,” amesema
Aidha, amesema watahiniwa 4,679 ni wenye mahitaji maalum, wakiwemo wasioona 92, wenye uoni hafifu 1,551, uziwi 1,079, ulemavu wa akili 448 na ulemavu wa viungo 1,509.
Ameeleza kuwa masomo yatakayofanyiwa mtihani huo ni sita Kiswahili, English Language, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, pamoja na Uraia na Maadili.
“Mtihani huu ni muhimu kwa kupima uelewa wa wanafunzi na hutumika kama msingi wa kuwachagua watakaojiunga na elimu ya sekondari,” amesema Profesa Mohamed.
Kuhusu maandalizi, Katibu Mtendaji huyo amesema tayari karatasi za mtihani na nyaraka zote muhimu zimesambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ikiwa ni pamoja na vifaa kwa ajili ya watahiniwa wenye mahitaji maalum.
“Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu, ikiwa ni pamoja na kutoa semina kwa wasimamizi wa mitihani na kuhakikisha mazingira ni salama na huru dhidi ya udanganyifu,” amesisitiza
Hata hivyo ametoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia mtihani kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.
“Wasimamizi wanapaswa kuhakikisha kuwa, wanafanya kazi ya usimamizi wa mtihani huu kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake. Wasimamizi wahakikishe watahiniwa wote wanafanya mtihani kwa muda uliopangwa na katika hali ya utulivu,”amesisitiza Profesa Mohamed.
Ameongeza kuwa wasimamizi wanapaswa kuhakikisha watahiniwa wenye mahitaji maalum wanapata haki zao za msingi.
Amesema haki hizo ni pamoja na kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu na waongezewe muda wa dakika ishirini (20) kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika kumi (10) kwa kila saa kwa masomo mengine, kama mwongozo wa baraza unavyoelekeza.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako