Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Songwe



MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame, ametoa onyo kali kwa wananchi na kamati za ulinzi na usalama kuhakikisha miradi ya umwagiliaji inalindwa dhidi ya vitendo vya hujuma, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni uti wa mgongo wa mapambano dhidi ya umaskini kwa wakulima.
Makame alitoa kauli hiyo wakati akikabidhi eneo la ujenzi kwa mkandarasi wa mradi wa skimu ya umwagiliaji wa Naming’ongo, kata ya Chitete, wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 24 unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC).
“Fedha hizi ni nyingi na zimekusudiwa kumwinua mkulima. Yeyote atakayehujumu miradi hii anahujumu Taifa, na lazima achukuliwe hatua. Ni jukumu letu sote kulinda miundombinu hii,” alisema Makame.



Mradi huo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya watu 2,000 na kuwanufaisha wakulima zaidi ya 6,000, huku ukipanua eneo la umwagiliaji kutoka hekta 1,500 hadi hekta 5,000. Pia utahusisha ujenzi wa barabara za ndani, ghala la kuhifadhi nafaka na mashine za kuchakata mazao, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao na kuinua kipato cha wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, alisema miradi ya umwagiliaji ni miradi ya kimkakati inayolenga kubadilisha maisha ya wananchi na kuchochea kilimo cha biashara.
“Tulitegemea mvua zisizo na uhakika, sasa tunapata kilimo cha uhakika kitakachoongeza uzalishaji na kuchochea uchumi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa, alisema zaidi ya miradi 700 ya umwagiliaji inaendelea kutekelezwa nchini kote, ikiwemo mabonde 22 yaliyochaguliwa kimkakati.


“Serikali imewekeza zaidi ya trilioni 1.2 katika sekta hii. Zaidi ya miradi 30 imekamilika, na mingine zaidi ya 60 ipo zaidi ya nusu ya utekelezaji. Lengo letu ni kuiwezesha Tanzania kulisha dunia,” alisema.
Mhandisi wa NIRC mkoani Songwe, John Chacha, alieleza kuwa mradi wa Naming’ongo utaongeza tija ya uzalishaji wa mpunga kutoka tani 2.4 kwa hekta hadi kufikia tani 25 kwa hekta.
Mwenyekiti wa skimu hiyo, Kredo Siwiti, aliishukuru serikali kwa uwekezaji huo mkubwa na kuahidi ushirikiano wa wananchi kuhakikisha mradi unakamilika kwa mafanikio.




More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama