Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza
Wajasiriamali wa sekta ya utengenezaji wa keki wametakiwa kurasimisha biashara zao na kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha ili kuhakikisha usalama wa walaji na kujiinua kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Ofisa Maendeleo wa Jiji la Mwanza, Erica Stephen, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji, Wakili Kiomoni Kibamba, wakati akifungua maonesho ya kwanza ya keki ya kihistoria Kanda yanayofanyika jijini Mwanza.

“Serikali inaendelea kuwainua wananchi kiuchumi, hususani wajasiriamali,ili mfanye kazi kwa uhuru na kupata fursa zaidi, ni muhimu kurasimisha biashara zenu,”amesema Erica.
Amesema Idara ya Maendeleo ya Jamii imepewa dhamana ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, huku akisisitiza kuwa maonesho hayo ni jukwaa la kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujitangaza na kupanua wigo wa masoko.
“Tujitahidi kurasimisha biashara, tuzingatie ubora kwa afya za walaji na kuhakikisha huduma kwa wateja inazingatia muda. Kujitangaza ni muhimu, watu hawawezi kufahamu unachofanya kama hujajitangaza,” amesema Erica.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya BJ Empire iliyoandaa maonesho hayo, Benard James, amesema tukio hilo ni la kihistoria kwani ni mara ya kwanza kwa sekta ya waokaji keki kupewa jukwaa kubwa Kanda ya Ziwa na nchini.
“Lengo letu ni kuipa sekta hii hadhi, kuiinua na kuikuza ili iweze kutoa mchango zaidi katika maendeleo ya taifa. Kwa kushirikiana na serikali, tunaamini ukuaji wa sekta hii itapunguza changamoto ya ajira nchini,” amesema James.
James amesema,amaonesho hayo yameleta mwelekeo mpya katika sekta ya uokaji ambapo kabla, waokaji walipatiwa mafunzo ya uendeshaji na usimamizi bora wa biashara,utengenezaji wa keki kwa viwango vya kisasa, usajili wa biashara na udhibiti ubora wa bidhaa kupitia taasisi za BRELA,SIDO,TBS na VETA,
Baadhi ya wajasiriamali walioshiriki, akiwemo Aurelia Aristedes na Lina, wameeleza furaha yao kushiriki maonesho hayo huku wakibainisha mafanikio na changamoto zinazowakabili.

“Maonesho haya yametufungua macho, tukipata mikopo isiyo na riba kutoka serikalini itatuepusha na mikopo ya kausha damu.Kupitia maonesha haya tutapata wateja wapya na kujifunza kwa wengine lakini ipo changamoto yawateja kuahirisha kuchukua oda,”amesema Aurelia.
Lina amesema,“Biashara yangu inakua kwa kasi, lakini gharama za vifaa na mabadiliko ya bei ya mara kwa mara ni changamoto. Kukatika kwa umeme wakati wa kutengeneza keki kunasababisha hasara,”.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina