Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mgombea wa Urais wa CCM,Dkt. Samia Suluhu Hassan,ameendelea kuchanja mbunga kusaka kura za kuomba dhamana ya utumishi kwa watanzania katika nafasi ya Urais.
Ambapo jana Agosti 3,2025 amefanya mikutano mikubwa ya kampeni katika
majimbo ya Tunduma na Vwawa mkoani Songwe.
Dkt. Akiwa Tunduma aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kwenye
mkutano wa kampeni, na hasa vijana kwa mshikamano wao mkubwa.
Amewaeleza wananchi kuwa safari ya maendeleo itaendelea kwa kasi
zaidi endapo watamchagua tena kuongoza nchi katika kipindi cha
2025-2030.
Ameahidi kuendeleza sekta za elimu, afya, maji na umeme kwa kuongeza
shule, kuendeleza sera ya elimu bila ada, na kuongeza mikopo kwa
wanafunzi ili vijana wote wapate fursa ya masomo.
Aidha, ameahidi kujenga vyuo vya VETA katika mkoa wa Songwe, ili vijana wapate ujuzi na kujiandaa kwa ajira na kujiajiri. Kuhusu afya, alisisitiza kuwa hospitali
mpya, vituo vya afya na zahanati zaidi vitajengwa ili wananchi wapate
huduma karibu na makazi yao.
Kwa upande wa maji, Dkt. Samia ameahidi kumaliza miradi mikubwa ya
maji, kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na
salama, kufikia asilimia zaidi ya 90 upatikanaji vijijini na mijini. Vilevile,
alisema kuwa kila kaya itapatiwa huduma ya umeme na kuongeza
kuwa ahadi yake ya Bima ya Afya kwa Wote tayari imeanza kufanyiwa
majaribio, ambapo serikali itabeba gharama za matibabu kwa wale
wasio na uwezo.
Akizungumzia miundombinu, ameeleza kuwa maboresho makubwa
yaliyofanyika Bandari ya Dar es Salaam yameongeza tani ya mizigo
inayopita Tunduma, na sasa serikali imeanza kukarabati barabara kuu
ya TANZAM.
Ameahidi kukamilisha kipande cha Igawa–Tunduma na Songwe–Tunduma (km 75) na kuendelea na vipande vilivyosalia,
sambamba na kuimarisha reli ya TAZARA ili iwe ya kisasa zaidi na iweze
kubeba mizigo kwa haraka.
Aidha Dkt. Samia,ameahidi kukamilisha ujenzi wa bandari kavu kubwa ya
ekari 1,800 eneo la Katenjele, kata ya Mpemba, ili kuondoa msongamano wa malori barabarani.
Pia, barabara mbadala
zitajengwa, sambamba na maegesho ya kisasa na mizani mpya.
Amesisitiza pia kwamba atahakikisha nyaraka za mizigo zinachakatwa
mapema kabla ya kufika mpakani ili kupunguza muda wa kusubiri. Dkt.
Samia alisema atazungumza na Zambia kuhakikisha nao, kupitia
mamlaka ya mapato, wanafanya kazi saa 24 ili wananchi wapate
huduma kwa haraka.
Dkt. Samia Kuhusu nishati, amewaomba wananchi wa Tunduma kumpa kura nyingi za ndiyo ili akamilishe mradi wa umeme mkubwa wa KV 730 kutoka Iringa, Njombe hadi Songwe, ambapo KV 430 zitatumika
Songwe na kV 300 zitaelekezwa Zambia.
Amebainisha kuwa mazungumzo
ya kuuza umeme yameanza na kwa wakati huo huo serikali yake itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi majumbani ili kuboresha maisha ya wananchi.
Akiwa katika jimbo la Vwawa,Dkt. Samia Suluhu aliwahutubia
wananchi katika mkutano uliofanyika Vwawa.
Katika mkutano huo
aliahidi kukamilisha ujenzi wa barabara muhimu ya Kamsamba na
kuhakikisha wilaya zote zinaunganishwa na barabara za lami hadi
makao makuu ya mkoa.
Kuhusu sekta ya kilimo, Dkt. Samia ameeleza kuwa changamoto ya
upatikanaji wa mbolea iko mbioni kutatuliwa kwani mbolea ya
kupandia tumbaku na mazao mengine tayari imeingia na ipo kwenye
hatua ya kusambazwa.
Ametumia nafasi hiyo kupongeza wakulima kwa
mafanikio makubwa, akibainisha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji wa chakula, hususan mahindi, na kwamba
taifa lina kiwango cha asiimia 128 cha utoshelevu wa chakula.
Amesema
mafanikio haya yamechochewa na mpango wa ruzuku ya pembejeo
unaotekelezwa na serikali ya CCM.
Kuhusu nishati, alibainisha kuwa umeme si changamoto kubwa tena
Songwe, lakini ataendelea na mkakati wa kujenga njia mpya ya
kusafirisha umeme yenye uwezo wa kV 730. Kati ya hizo, kV 430
zitatumika katika mikoa ya kusini, huku kV 300 zikielekezwa Zambia kama
sehemu ya mpango wa biashara ya nishati.
Amesisitiza pia umuhimu wa
nishati safi na akaahidi kuialika sekta binafsi kushiriki katika kujenga vituo
vya kusambaza nishati hiyo.
Kwa upande wa vijana, aliahidi kuendeleza fursa kwao kupitia mikopo
ya elimu na ujenzi wa vyuo vya VETA katika mkoa wa Songwe.
Amesema kuwa ada na gharama za mafunzo hayo zitabebwa na
serikali, ili kuhakikisha vijana wote wenye nia na uwezo wa kusoma
wanapata nafasi ya kupata ujuzi na hatimaye ajira.

More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro