March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Oryx gas yatoa elimu matumizi nishati safi kwa chama cha Skauti

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dodoma

KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania imesema inajivunia udhamini wake kwa kambi ya Skauti Tanzania, ikiwa ni dhamira ya kuendeleza vijana, kulinda mazingira, na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Pia kampuni hiyo imetoa mitungi ya gesi 260 mikubwa na midogo kwa chama hicho cha Skauti nchini.

Akizungumza Septemba 3,2025 katika kambi ya mafunzo ya Skauti Tanzania, iliyohusisha vijana skauti kutoka mikoa yote nchini,Meneja Mauzo wa kampuni hiyo Tanzania Bara,Alex Wambi,amesema kuwa hiyo ni hatua muhimu katika safari ya kuelekea matumizi ya nishati safi na kuwawezesha vijana.

Aesema utoaji wa mitungi hiyo ya gesi ni ishara ya imani, maadili ya pamoja, na dhamira ya kujenga mustakabali salama na wenye matumaini.

“Hii ni mara ya kwanza kwa kambi za skauti kutumia gesi. Skauti walikuwa na jukumu la kutafuta kuni za kupikia kwa kambi zote na kwa mara ya kwanza Oryx wamebadilisha maisha ya kambi hizo,”amesema.

Pia amesema Oryx gas inaamini katika nguvu ya mabadiliko inayotokana na vijana ambapo kambi hiyo ni darasa hai hivyo Skauti watajifunza jinsi ya kutumia gesi ya LPG kwa usalama, kuelewa faida zake na kuwa mabalozi wa nishati safi katika maeneo yao.

“Tunatarajia kuona Skauti wakiongoza kampeni za kupikia kwa usafi, wakiratibu maonesho ya jamii, na wakijumuisha usalama wa LPG katika mafunzo yao.Pia kitatumia ushirikiano huu kama daraja la kuongeza wigo wa elimu, kuimarisha ushirikiano, na kuhamasisha mashirika mengine ya vijana kuiga mfano huu,”amesema Wambi.

Kwa upande wake Peter Ndomba ambaye ni Meneja wa miradi ya suluhisho la nishati safi kutoka Oryx Gas,amesema kupitia kambi hiyo wataitumia kama sehemu ya dhamira yake ya kuendeleza vijana, kulinda mazingira, na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Ndomba amesema lengo la mafunzo hayo ni kusaidia maandalizi ya chakula wakati wote wa kambi pamoja na kuhakikisha mazingira yasiyo na moshi yanayoendana na viwango vya kisasa vya nishati safi.

“Tunaamini katika kuwawezesha viongozi wa kesho kwa kuwapatia maarifa na nyenzo za maisha endelevu.Udhamini wetu kwa Skauti Tanzania unaendana na dhamira yetu ya kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuhamasisha matumizi bora ya nishati miongoni mwa vijana na jamii,”amesema Ndomba.

Pia amesema wataendesha vipindi vya elimu kuhusu usalama, ufanisi wa nishati, na mchango wa kupikia safi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Juhudi hizo ni sehemu ya kampeni pana ya kuelimisha jamii kuhusu faida za LPG na kuhimiza matumizi yake katika maeneo ya mijini na vijijini.