March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askari polisi wawili na wengine watano mbaroni tuhuma wizi wa mbolea

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online-Songwe.

Jeshi la Polisi mkoani Songwe linawashikilia watu saba, wakiwemo askari polisi wawili, kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mifuko 534 ya mbolea aina ya UREA yenye thamani ya zaidi ya milioni 45.4.

Mbolea hiyo ni mali ya kampuni ya Ocean Network ya nchini Zambia, ilikuwa inasafirishwa kwa njia ya reli kutoka Dar-es-Salaam kuelekea nchi jirani ya Zambia, kabla ya kuibwa usiku wa Agosti 19, 2025 katika Kijiji cha Nanyala, Wilaya ya Mbozi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, akizungumza na waandishi wa habari Septemba 2, 2025,amesema watuhumiwa hao walishirikiana kwa kupanga njama na kusimamisha treni yenye usajili wa namba 0139A mali ya TAZARA,eneo lisilo rasmi kwa ajili ya kushusha mbolea hiyo.

Amesema watuhumiwa hao ni pamoja na madereva wa treni na wafanyabiashara wa mbolea, huku askari wawili waliokuwa wakisindikiza treni hiyo nao wakihusishwa moja kwa moja na tukio hilo.

Hata hivyo, Kamanda Senga hakuwa tayari kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa sababu za kipelelezi.

Pia Senga,amesema katika msako uliofanyika, Polisi walifanikiwa kukamata mifuko 134 ya mbolea hiyo kwenye nyumba ya mmoja wa watuhumiwa katika Kijiji cha Ipoloti, Kata ya Bara wilayani Mbozi.

Hata hivyo amesema, uchunguzi unaendelea ili kubaini wahusika wengine na magari yaliyotumika kubeba mbolea hiyo, akisisitiza kuwa wote waliohusika watakabiliwa na mkono wa sheria.

“Hili ni tukio la kihalifu linalohusisha mtandao mpana wa watu,hivyo tunafanya uchunguzi wa kina na tutahakikisha wote waliohusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema Senga.