Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha


BENKI ya Exim imepanua huduma yake ya kifahari ya Elite Banking hadi kanda ya kaskazini, ikiwa ni baada ya mafanikio ya uzinduzi wake jijini Dar es Salaam mapema mwaka huu. Huduma hiyo inalenga kutoa huduma za kifedha za kisasa na za kibinafsi kwa wateja wa kipato cha juu katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Shani Kinswaga, alisema huduma ya Elite Banking ni hatua ya benki hiyo “kufafanua upya dhana ya upekee katika huduma za kifedha nchini”.
“Huduma hii siyo tu akaunti ya kibenki, bali ni ahadi ya kuwa karibu na mteja. Tunawaletea suluhisho za kifedha za kisasa, ushauri wa kitaalamu na huduma zinazobeba ndoto na matarajio ya kila mmoja wao,” alisema Kinswaga wakati wa hafla ya uzinduzi.

Kwa mujibu wa benki hiyo, Elite Banking inawapa wateja manufaa kadhaa ikiwemo: maeneo maalum ya mapokezi ndani ya matawi, usimamizi binafsi wa mahusiano na washauri wa kifedha, huduma za kidijitali zenye urahisi na usalama zaidi, pamoja na fursa za kimataifa kupitia ushirikiano na kampuni ya Mastercard.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Rejareja wa Exim, Bw. Andrew Lyimo, alibainisha kuwa huduma hiyo “imeundwa kuendana na malengo ya kifedha ya wateja na kuwapatia safari ya kibenki isiyo na usumbufu”.
Kupitia ushirikiano na Mastercard, wateja wa Elite Banking watapata kadi tatu maalum za kimataifa (World Debit TZS, World Debit USD na World Credit Card), zinazotoa manufaa ya kipekee kama vile ufikiaji wa zaidi ya 1,000 VIP lounges katika viwanja vya ndege duniani, bima kamili ya safari, pamoja na ulinzi wa hali ya juu wa manunuzi.
Kwa hatua hii, Exim Bank imeimarisha nafasi yake kama benki ya kwanza nchini kuunganisha huduma za kifedha za ndani na fursa za kifahari za kimataifa, na hivyo kuleta ushindani mpya katika sekta ya kibenki Tanzania.




More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama