March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bonah:Barabara Jimbo la Segerea kujengwa kiwango cha lami

Na Heri Shaaban, Timesmajira Online Dar es Salaam

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Segerea Bonnah Ladslaus Kamoli (CCM),amesema barabara zote ndani ya Jimbo hilo zitajengwa kwa kiwango cha lami.

Ambapo itakuwa ni utekelezaji wa ilani ya chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia mradi wa DMDP ambao umeanza kutekelezwa jimboni humo.

Bonaha mesema hayo katika uzinduzi wa kampeni ya Jimbo la Segerea uliofanyika uwanja wa Liwiti wilayani ya Ilala mkoani Dar-es- Salaam,ambapo mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Ally Hapi.

Amesema,katika Jimbo la segerea wananchi waliteseka kwa muda mrefu kwa sababu ya miundombinu ya barabara kuwa mibovu,hivyo amempongeza Dkt.Samia suluhu Hassan kwa kutekeleza ilani ya CCM jimboni humo.

“Mradi tuliokuwa tunasubiri kwa hamu wa kuboresha miundombinu ya Jiji (DMDP) tayari umeanza Wakandarasi wapo kazini,barabara zinajengwa za kisasa ikiwemo ya Kinyerezi-Bonyokwa,Segerea-Bonyokwa,Segerea-Zahanati,Tabata Mwananchi na Kimanga.Nipigieni kura mimi na wagombea wote wa CCM akiwemo Rais,”amesema Bonah.

Pia amesema kwa sasa wananchi wa Jimbo la Segerea wanapata maji kwa asilimia 90 ikiwemo Kata ya Kinyerezi na Bonyokwa ambao awali walikuwa hawapati huduma hiyo vizuri.

Hata hivyo amesema,Rais Samia,ametekeleza ilani ya CCM katika sekta ya afya jimboni humo ambapo vituo vya afya vimejengwa kikiwemo cha Kinyerezi,Segerea na Kiwalani ambavyo kwa sasa vituo vyote vinatoa huduma ya matibabu.

Aidha amesema katika sekta ya elimu ilani ya CCM imetekelezwa pia ambapo shukr za sekondari zipo za kutosha na miundombinu imeboreshwa kuanzia shule za msingi.

Vilevile amesema,wananchi wamewezeshwa kiuchumi kupitia mikopo ya Serikali inayotolewa kupitia asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri.

Kwa upande wake mgombea Udiwani Kata ya Vingunguti wilayani Ilala,aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar-es-Salaam Omary Kumbilamoto,amesema mgombea Ubunge huyo ana mchango katika maendeleo ya Jiji hilo.

Amesema Jiji hilo limeingiza kiasi Cha bilioni 317,katika fedha hizo Bonah ana mchango wake,pia amefanya juhudi na kuhakikisha Kata ya Liwiti imepata shule ya sekondari ya kisasa vilevile Kata ya Buguruni.

Hivyo amewahimiza wananchi kuchagua wagombea wanaotokana na CCM kwa nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Ally Hapi amesema Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya makubwa katika sekta ya afya,elimu na miundombinu ya barabara ya kisasa.

.