March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali,Oryx Gas zanogeshabiashara ya samaki soko la Feri

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online-Dar

SERIKALI kwa kushirikiana na kampuni ya ORYX Energies Tanzania na wadau wa soko, imetangaza uzinduzi wa mfumo wa kwanza wa usambazaji wa gesi ya LPG kwa wingi katika soko la samaki la kimataifa Feri jijini Dar-es-Salaam.

Mradi huo wa kihistoria ni hatua kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa nishati safi kwa wauzaji wa samaki na wajasiriamali wadogo katika soko hilo ,ambapo kwa mfumo huo unaweza kulipia kadri ya matumizi (PAYG).

Mfumo huo unaowawezesha wauzaji samaki kulipia gesi wanayotumia tu na hivyo kuondoa gharama kubwa za kujaza mitungi na kupunguza matumizi ya kila siku hadi sh.45,000.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo huo ambapo limejengwa tanki kubwa ambalo linatumika kusambaza gesi katika majiko ya wafanyabiashara hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam, Albert Chalamila amesema mfumo huo utawezesha kulipa kulingana na matumizi ya mhusika.

Chalamila amesema, ajenda ya kuwa na matumizi ya nishati safi ya kupikia ilikuwepo tangu zamanı ingawa mkazo wake ulikuwa mdogo, lakini Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameibeba ajenda hiyo na Oryx Energies wameonesha kwa vitendo kuunga mkono jitihada hizo kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.

“Wenzetu Oryx Energies wameendelea kujitoa katika eneo hili la nishati safi ya kupikia kwa kuja na mfumo huu ambao sasa unakwenda kurahisisha upatikanaji gesi katika soko hili la samaki Feri.

Amesema katika soko la samaki Feri kuna majiko ya wakaanga samaki 48,na sasa wote wameunganishwa katika mfumo huo wa gesi, na wanaamini matumizi ya nishati safi ya kupikia yanakwenda kundoa changamoto za kiafya za watumiaji wakiwemo wanawake ambao wanafanya shughuli zao katika soko hilo.

Pia amesema, matumizi ya nishati safi ya kupikia hayaokoi tu afya za watumiaji bali hata gharama za uendeshaji zinapungua kwa asiliamia kubwa, ambapo mradi huo umegharimu zaidi ya milioni 250 na
matamanio yake ni kuona masoko yote yalipo katika Jiji la Dar-es-Salaam yanakuwa na mfumo huo.

Hata hivyo amewataka wadau wote wa nishati safi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hususani kwa kuyafikia masoko yote huku lengo nikuona afya za watu zinakwenda kuwa salama .

Huku amesisitiza kuwa hawazindui tu miundombinu bali wamezindua mabadiliko ya kweli katika usalama, ufanisi, na ustawi wa kila mfanyabiashara anayefanya kazi sokoni hapo.

Hata hivyo amesema,kila mfanyabiashara sasa ana mita yake inayosoma matumizi yake ya kila siku, kabla na baada ya matumizi. Hakuna tena kubahatisha, hakuna tena kulazimika kununua mitungi midogo kwa gharama kubwa.

Kadhalika amesema, Oryx wamezingatia usalama kwa kufunga valve ambazo itatumika kufunga gesi endapo itatokea dharura kwa kila jiko. “Tunafahamu matumizi makubwa hivi ya gesi yanahitaji usalama wa hali ya juu.

Nafahamu kwamba Oryx mtaendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya huu mfumo ili kuepusha ajali yoyote inayoweza kutokea kwa kutokujua au kupuuzia kanuni sahihi za usalama,”amesema Chalamila.

Sanjari na hayo amesema viwango vya matumizi gesi vitafuatiliwa kwa urahisi ili kuhakikisha gesi inajazwa kwenye tanki kubwa kwa wakati huku akieleza kuwa harama imepungua na wafanyabiashara waliokuwa wakitumia hadi sh.180,000 kujaza gesi kwa siku sasa wanaweza kuokoa hadi sh.45,000 kila siku.

Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas,Benoit Araman,amesema lengo la kuwa na mfumo huo wa tanki la gesi katika soko hilo unalenga kupunguza gharama za kujaza, kupunguza upotevu, na kuongeza ufanisi,usalama na mfumo usiovuja.

Amesema ni mfumo wa kisasa uliofanywa na timu ya ufundi ya Oryx Gas kwa kuzingatia kanuni za kitaifa na kimataifa,urahisishaji wa uendeshaji ugavi endelevu,ufuatiliaji wa kisasa pamoja na matengenezo madogo.

Benoit amesema, Oryx Energies imejipanga kuunga mkono Mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa 2024–2034, kwa kusambaza mfumo huo katika masoko ya samaki ya Zanzibar, Mwanza, na mikoa mingine.

“Kampuni pia inaendelea kuunganisha mifumo ya LPG kwa wingi shuleni, taasisi, majengo ya biashara na viwandani nchini kote,mradi huu si miundombinu tu ni ahadi ya kuinua jamii, kulinda mazingira, na kuchochea ukuaji wa uchumi,”amesema.

Kamishina wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga,amesema tangu mkakati wa kitaifa ulipozinduliwa Januari ,mwaka 2024 wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kumekuwa na mafanikio makubwa na ongezeko la matuminizi ya majiko ya gesi.

Mhandisi Luoga,amesema mkakati wa Serikali ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Ili kufikia malengo hayo ya mkakati ni taasisi au makundi makubwa yanayolisha watu kwa pamoja wanahamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na katika hili maeneo mengi tayari yameaza kufikiwa.

Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Zungu, amesema awali wafanyabiashara wa soko hilo walimfikishia mahitaji yao hivyo aliwatafuta Oryx Gas na leo amefurahi kuona umefungwa mfumo huo ambao unakwenda kurahisisha shughuli za wafanyabiashara hao.

Zungu ameaema tafiti zinaonesha duniani kuwa kuna vifo vingi vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo salama, hivyo mradi huo unakwenda kuwa na majawabu ya kuimarisha afya za wadau hao.