Na Mwandishi wetu,Timesmajira
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuzingatia maadili ya taaluma yao kwa kuandika habari za ukweli, na kuepuka uchochezi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Octoba mwaka huu.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam Agosti 14, 2025 na Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni ya Media Brains, Absalom Kibanda, wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari, yaliyoandaliwa na Kampuni ya Media Brains kwa udhamini wa Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) kutoka Ujerumani.
Amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu waandishi wa habari wanapaswa kujiepusha na kuandika habari zinazoegemea upande wowote au zenye uchochezi na ushabiki.
“Uandishi wa habari salama ni ule unaosimamia ukweli, misingi ya taaluma bila kuegemea upande wowote.katika kipindi hiki waandishi wa habari mnapaswa kusimamia misingi ya taaluma” amesema

Aidha amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uandishi wa habari za uchaguzi kwa usahihi, weledi na kulinda amani ya taifa.
Naye Mkurugenzi wa Media Brains, Neville Meena aliwawataka waandishi wa habari kuandika habari kwa usahihi wakati wa kipindi cha uchaguzi na kwamba wasipofanya hivyo watajikuta katika matatizo makubwa.
“Hivi karibuni Bunge lilipitisha Sheria mbili na kufanya marekebisho makubwa katika sheria ya vyama vya siasa hivyo tumeamua kuandaa mafunzo haya li kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika sheria hizo.

“Waandishi wa habari tunapaswa kufanyakazi zetu kwa mujibu wa sheria, zipo sheria zinazohusu uchaguzi na zingine zinatugusa sisi waandishi moja kwa moja yaani maadili na miiko yetu hivyo tumekutana ili kukumbusha sheria hizi ili tufanyekazi zetu kwa weledi,” amesema Meena
Aidha amesema Kampuni ya Media Brains tayari imeshatoa mafunzo kama hayo kwa waandishi wa habari waliopo katika mikoa ya Mbeya, Kigoma, Mwanza, Kilimanjaro, Pwani na Morogoro.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako