March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi 24,000 Tabora wapewa elimu ya ukatili wa kijinsia

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora

HALMASHAURI ya Manispaa ya Tabora imetoa elimu juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi zaidi ya 24,000 wa shule za msingi na sekondari kwa mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo,Mohamed Masudi,wakati akizungumza na mwandishi wa wa Timesmajira aliyetaka kufahamu mikakati ya halmashauri ya kutokomeza ukatili wa kijinsia miongoni mwa jamii.

Amesema halmashauri imekuwa mstari wa mbele kupambana na kutokomeza vitendo hivyo kwa kuzingatia mwongozo wa uratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II).

Ambapo amesema,sababu kuu ya vitendo hivyo kuwa ni uchumi duni kwa baadhi ya kaya na matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia na mitandao ya kijamii huku Halmashauri imechukua hatuna ya kukabiliana na vitenfo hivyo kwa kutoa elimu na mikopo wezeshi

Masudi ameeleza kuwa juhudi hizo zimewezesha wataalamu wa halmashauri hiyo kutembelea jumla ya shule za msingi 82 na za sekondari 31 na kutoa elimu kuhusu ukatilimkwa wanafunzi 24,501.

Kati ya wanafunzi hao wasichana ni 14,180 na wavulana 10,321 huku wananchi wengine ni 18,941 ambapo wanaume ni 8,041 na wanawake 10,900, elimu hiyo imetolewa kupitia mikutano ya hadhara katika kata zote 29 za manispaa hiyo.

Katika kuhakikisha uchumi wa kaya maskini unaimarishwa, amesema halmashauri hiyo imetoa mikopo nafuu ya jumla ya bilioni 2.18 kwa vikundi 163 kupitia asilimia 10 ya mapato yake ya ndani.

Aidha wametoa mikopo ya milioni 12.5 kwa wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga) kupitia benki ya NMB na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya teknolojia na mitandao ya kijamii kupitia midahalo na mafunzo.

Masudi ameongeza kuwa pia wamefanikiwa kusikiliza migogoro 238 kwa wananchi wapatao 10,955,kati yao wanaume wakiwa 5,242 na wanawake 5,713 kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid.

Migogoro 193 imetatuliwa, 33 ipo katika hatua za utatuzi na 12 imewasilishwa kwenye mamlaka nyingine, aidha walipokea wahanga 13 wa ukatili wa kijinsia katika kituo cha afya maili tano na kuwapa huduma inayostahili kwa wakati.