Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na PETPRO wameweka historia kwa kusaini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kuzindua mfumo wa kwanza wa kitaifa wa ukusanyaji na urejelezaji wa chupa za kioo baada ya matumizi nchini.
Mpango huu wa kimkakati unalenga kukabiliana na changamoto ya usimamizi wa taka za chupa za kioo, huku ukichangia uhifadhi wa mazingira na kuimarisha uchumi wa taifa. Mfumo huo utapunguza kwa kiwango kikubwa taka zinazotupwa dampo, kuongeza viwango vya uchakataji na kubadilisha taka kuwa malighafi zenye thamani. Hatua hii pia inaendana na mkakati wa maendeleo endelevu wa TBL kwa mwaka 2025.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, amesema ushirikiano huo ni mfano wa kuigwa unaoendeleza uwajibikaji wa mazingira, ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii. “Tunafurahi kwa fursa hii inayotuwezesha kubadilisha taka za chupa za glasi kuwa fursa, huku tukisaidia jamii husika na kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PETPRO, Nicholaus Jackson, amesema ushirikiano huo unaweka kiwango kipya cha uchakataji wa taka za kioo nchini. “Uzoefu wetu wa pamoja utahakikisha tunakusanya na kuchakata kwa njia endelevu, tukileta matokeo chanya kwa uhifadhi wa mazingira na kutoa fursa za kiuchumi kwa Watanzania,” amesisitiza.

Mradi huu unatarajiwa kuleta fursa za ajira na kipato kwa wakusanyaji taka, wachakataji na wazalishaji, hususan katika jamii zenye uhitaji mkubwa, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi, serikali na wadau wengine kuelekea uchumi wa mzunguko.
Hati ya Makubaliano hii inathibitisha nafasi ya TBL na PETPRO kama vinara katika mapinduzi ya uchakataji wa chupa za kioo nchini, na kuwa mfano wa kuigwa kwa sekta nyingine.

More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro