March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Itracom yapongeza juhudi za kuboresha sekta ya kilimo

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora

KAMPUNI ya Itracom imepongeza Serikali kwa kuboresha sekta ya kilimo nchini na kufungua milango kwa wawekezaji kuanzisha kampuni za uzalishaji mbolea yenye virutubisho vya udongo kwa bei nafuu.

Pongezi hizo zimetolewa mjini hapa na Ofisa Mwandamizi na Mtafiti wa kampuni ya Itracom Fertilizers Ltd inayozalishaji mbolea ya asili ya fomi, Nsabiyumva Macedoni, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii.

Amesema kuwa hatua ya serikali kutoa fursa kwa kampuni hiyo kuanza kuzalisha mbolea ya asili yenye samadi na virutubisho vya udongo itasaidia wakulima kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji wa mazao yao mara dufu.

Amebainisha kuwa mbolea ya fomi ambayo huzalishwa kwa malighafi ya asili, chokaa na virutubisho imeanza kuleta mageuzi kwa wakulima katika mikoa mbalimbali baada ya kuanza kutolewa na serikali kwa mfumo wa ruzuku.

Macedoni,amefafanua kuwa uzalishaji wa mbolea hiyo umeendelea kuongezeka kila mwaka na hadi sasa wanazalisha takribani tani milioni 1kwa mwaka, na kuzisambaza katika mikoa yote hadi maeneo ya vijijini.

Amedokeza kuwa kwa sasa wanazalisha mbolea aina tatu za fomi ikiwemo kwa ajili ya kuoteshea mazao yote,kukuzia mazao yote na ya kunenepesha mazao ya mizizi, bustani na matunda.

Aidha wako mbioni kuanza uzalishaji wa aina zingine 11 za mbolea kwa ajili ya matumizi tofauti ikiwemo fomi asili ambayo haina kemikali ndani yake ili kupanua wigo kwa wakulima kutumia mbolea wanayotaka.

Afisa Kilimo wa kampuni hiyo anayesimamamia Mkoa wa Kigoma, Christopher Peter Mihayo ameeleza kuwa mbolea hiyo ni mkombozi kwa kuwa inasaidia sana kurutubisha udongo uliochoka.

Ili kuhakikisha kilimo kinaendelea kuwa uti wa mgongo na kuinua maisha ya wakulima,wameendelea kuwapa elimu ya kilimo bora na matumizi sahihi ya mbolea hiyo na matokeo yameendelea kuwa chanya katika misimu yote.

Amebainisha faida zinazopatikana kutokana na matumizi ya mbolea hiyo kuwa ni mazao kustawi vizuri sana, kuongeza uzalishaji, kuboreshwa afya ya udongo, ardhi kutumika kwa muda mrefu, kuepusha ukataji miti na kupata ruzuku ya serikali.