Na Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara
SERIKALI mkoani Mara imeyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kushiriki kwa amani na utulivu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025, bila kuingiza masuala ya kisiasa yanayoweza kuleta mgawanyiko na chuki katika jamii.
Wito huo umetolewa Agosti 9, 2025 mjini Musoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika, katika mkutano wa tathmini ya mchango wa NGOs katika maendeleo ya taifa kwa kipindi cha 2020/2021 hadi 2024/2025.
Katika hotuba hiyo, RC Mtambi amesisitiza kuwa mashirika hayo yanatakiwa kuwa sehemu ya kuimarisha mshikamano, amani na upendo miongoni mwa Watanzania kwa kuwa misingi hiyo ni nguzo ya maendeleo ya taifa.

“Lazima NGOs zijipime. Zifanye kazi kwa bidii kukomesha mila na desturi potofu. Nasikitika kuona watoto bado wanakeketwa. Himizeni watoto wasome na waelimike. Elimisheni jamii kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na ukeketaji, na vitendo hivyo vikomeshwe kabisa,” alisema Mkuchika kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa.
Pia, amezitaka NGOs kuhakikisha zinazingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi katika utekelezaji wa majukumu yao, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha ushirikiano na Serikali katika kuleta maendeleo.
“Hakikisha mnahimiza amani na umoja katika maeneo yenu. Nchi yetu imeendelea kuishi kwa amani. Lazima msisitize upendo na mshikamano,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Mara, Rhobi Samwelly, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, amesema mashirika hayo yamepiga hatua kubwa katika kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Tuna jukumu la kuendelea kupinga ukatili wa kijinsia kwa juhudi zote. Tutoe elimu kwa jamii, tuhimize watu kuwafichua wanaofanya ukatili, na tusaidie watoto wa kike na wa kiume kutimiza ndoto zao,” amesema Rhobi.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Mara, Neema Ibamba, amesisitiza umuhimu wa NGOs kuweka wazi mipango na bajeti zao ili kuhakikisha shughuli zao zinaeleweka na kuleta manufaa kwa jamii.”Mashirika haya yaendelee kushirikiana na Serikali na kuhakikisha yanatoa mchango chanya kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla,” amesema.

More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI