
*TFC KUSIMIKA KIWANDA CHA KUCHANGANYA NA KUTENGENEZA MBOLEA NCHINI*
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Samwel Mshote amesema kuwa, kampuni hiyo inatarajia kupokea mitambo kwa ajili ya kusimika kiwanda cha kuchanganya mbolea, kitakacholenga kuzalisha mbolea kulingana na mahitaji halisi ya udongo katika maeneo mbalimbali nchini.
Amebainisha kuwa tayari TFC imepata mbia kutoka Nchini Zambia atakayewekeza katika ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea kwa kutumia rasilimali zinazopatikana nchini, ikiwemo makaa ya mawe pamoja na madini ya phosphate kutoka mikoa ya Manyara na Songwe.
Aidha, kampuni hiyo imekwishapata ardhi yenye ukubwa wa ekari 2,750 katika Manispaa ya Tabora, ambapo maandalizi ya awali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa yameshaanza, huku lengo likiwa ni kuanza ujenzi mwaka huu.
Mpango huu ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha Tanzania inaanza kujitosheleza kwa uzalishaji wa ndani wa mbolea, kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi, na hivyo kuokoa fedha nyingi za kigeni. Vilevile, uanzishaji wa kiwanda hicho unatarajiwa kuchochea ajira kwa vijana, kukuza kipato cha wananchi mmoja mmoja, na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kwa upande mwingine, TFC imejipanga kusambaza tani 200,000 za mbolea kwa msimu huu, ikiwemo mbolea ya kupandia aina ya Diammonium Phosphate (DAP), Urea (N-46), na Calcium Ammonium Nitrate (CAN 27). Mbolea ya DAP na Urea tayari zimeanza kusambazwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini, huku shehena nyingine zikiwa njiani.
TFC pia ina vituo vikubwa vya mauzo katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Mwanza na Tabora, na inawakaribisha Watanzania wote wanaopenda kushiriki katika mnyororo wa usambazaji wa mbolea, kujitokeza ili kushirikiana kama mawakala wa mbolea katika maeneo yao.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi