Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
BODI ya Maziwa nchini imetumia fursa ya Maonyesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma kutoa mafunzo ya usalama na ubora wa maziwa kwa wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa huku ikiwaonya wananchi kununua maziwa yaliyofungashwa kwenye chupa za maji.
Akizungumza wakati wa maonyesho hayo katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma,, Mkurugenzi wa Chakula kutoka Bodi ya Maziwa Nchini Rajilani Hilla amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wazalishaji na wachakataji wa maziwa kubaini maziwa bora, salama na yasiyoharibika ili kulinda afya za walaji nchini.
“Tumelenga kuwafundisha wadau wetu namna ya kutambua na kuzalisha maziwa kwa njia za kitaalam. Pia tunawapatia mafunzo ya usindikaji wa mazao muhimu mawili ya maziwa, ambayo ni mtindi wa kawaida na mtindi wa kawaida unaotumika zaidi nchini,” alisema Bw. Hilali.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto ya kutowafikia Watanzania wote kutokana na uwezo mdogo wa taasisi, bado Bodi inatoa wito kwa wananchi kutumia maziwa yaliyosindikwa na yanayopatikana kwenye viwanda vya ndani ili kuepuka maambukizi na magonjwa yanayotokana na matumizi ya maziwa yasiyo salama.
“Mpaka sasa tuna viwanda 187 vinavyochakata maziwa nchini, vikijumuisha vidogo, vya kati na vikubwa. Tunawasihi wananchi waepuke kutumia maziwa yanayouzwa mitaani hasa yale yanayohifadhiwa kwenye vyombo visivyo salama kama vile machupa ya maji,” ameongeza
Bw. Hilali amesisitiza kuwa matumizi ya maziwa yasiyo salama huweza kuhatarisha afya ya mlaji kwa kiwango kikubwa, hivyo elimu ya usalama wa maziwa ni muhimu kwa kila mdau wa mnyororo wa maziwa kuanzia uzalishaji hadi mlaji wa mwisho.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi