Na Daud Magesa, Timesmajira Online-Mwanza
Watanzania wamehimizwa kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) ili kuwa na uhakika wa huduma bora za matibabu pindi wanapokumbwa na changamoto za kiafya.
Wito huo umetolewa na Ofisa Uanachama wa NHIF Mkoa wa Mwanza, John Munuo, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la mfuko huo katika maonesho ya Nane Nane Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika Nyamh’ongolo wilayani Ilemela jijini Mwanza,kikiwemo kikundi cha Greeting Earth kutoka Singida.
“Lengo la ushiriki wetu ni kutoa elimu ya bima ya afya,kusikiliza maoni mbalimbali ya wananchi. Rai yangu kwa Watanzania ni kuhakikisha wanakuwa na bima ya afya, iwasaidie katika maisha yao na kuwawezesha kupata huduma za matibabu pale wanapougua,” amesema Munuo.
Munuo ameeleza kuwa NHIF imeboresha mfumo wake wa usajili kwa kuanzisha huduma ya kujihudumia (self-service) kupitia tovuti maalum ya http://selfservice.or.tz
Kupitia mfumo huu, mwananchi anaweza kujisajili mwenyewe na wategemezi wake, kupata taarifa za matumizi ya bima, kupata kadi ya kielektroniki, kufuatilia michango yake, kupata orodha ya vituo vya kutolea huduma vilivyosajiliwa na kupata vibali na mrejesho wa huduma alizopata
“Kinachohitajika ni namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA). Baada ya kujaza taarifa na kujibu maswali muhimu, atapewa namba ya malipo (control number) kwa ajili ya kulipia kifurushi anachohitaji,” ameeleza Munuo.
Pia amesema,huduma hutolewa kulingana na aina ya kifurushi kilichochaguliwa, kuanzia huduma za msingi, kibingwa hadi ubingwa bobezi.
Munuo amezitaja faida za kujiunga na NHIF ni pamoja na matibabu kote nchini katika zaidi ya vituo 10,000 kuanzia zahanati hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili, punguzo la asilimia 10 kwa mchango wa mtegemezi katika kifurushi cha kifamilia.
Pia huduma za rufaa kwa kufuata utaratibu rasmi na kinga dhidi ya gharama kubwa za matibabu ya ghafla.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi