March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu ya ustawi wa wanyama yawafikia wafugaji Nanenane – LRCT yasisitiza haki na huduma bora kwa wanyama

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online – Dodoma

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imeweka mkazo katika kutoa elimu juu ya haki na huduma stahiki kwa wanyama wanaofugwa, kama sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu Sheria ya Ustawi wa Wanyama, Sura Na. 154. Elimu hiyo imetolewa kwa makundi mbalimbali ya wafugaji kutoka mikoa tofauti ya Tanzania wanaoshiriki katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Akizungumza Agosti 4, 2025, katika viwanja hivyo, Wakili wa Serikali kutoka LRCT, Vick Mbunde, alisema kuwa elimu hiyo inalenga kuwajengea ufahamu wafugaji kuhusu wajibu wao wa kisheria katika kuwahudumia vyema wanyama wao, kwa kuwapatia mahitaji ya msingi kama vile chakula, maji safi, malazi bora na huduma za tiba.

“Wafugaji wengi hawakuwa wakitambua kuwa kuwatesa wanyama wao ni kinyume cha sheria. Sheria ya Ustawi wa Wanyama inalinda wanyama dhidi ya mateso na manyanyaso, na inataka wamiliki wa wanyama kuwajibika kikamilifu katika malezi yao,” alieleza Vick.

Aliongeza kuwa Sheria hiyo, ambayo ipo chini ya Sura Na. 154, inaleta uwiano kati ya maendeleo ya sekta ya mifugo na ustawi wa viumbe hai, kwa kuhimiza matunzo yanayozingatia utu na haki za wanyama.

Katika banda la LRCT kwenye maonesho hayo, wananchi wamekuwa wakipata fursa ya kujifunza kupitia vipeperushi, maelezo ya moja kwa moja kutoka kwa wataalamu, pamoja na kuuliza maswali kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria yanayohusiana na mifugo na wanyama kwa ujumla.

Mfugaji Hosea Godwin, mmoja wa waliopokea elimu hiyo, alisema kuwa elimu hiyo imefungua macho yake na kumfanya atambue wajibu mkubwa alionao kwa wanyama anaowafuga.

“Nilikuwa sifahamu kuwa ukimwacha mnyama bila chakula au kumpiga ni kosa la kisheria. Sasa nimeelewa na nitakuwa makini zaidi. Hii ni elimu muhimu sana kwa wafugaji kama sisi,” alisema Hosea.

Tume ya Kurekebisha Sheria imeahidi kuendelea na kampeni hii ya utoaji wa elimu ya kisheria katika maeneo mengine nchini, ili kujenga jamii inayoheshimu sheria na kuhakikisha ustawi wa kila kiumbe hai unazingatiwa kwa mujibu wa sheria.