Na Penina Malundo,Timesmajira
KATIBU Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ)Mhandisi Zena Said amesema tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Uongozi imekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza uongozi kwa maendeleo endelevu barani Afrika.
Huku zaidi ya miaka 15 iliyopita Serikali ya Tanzania ilitambua umuhimu wa uongozi na maendeleo ya uongozi katika maendeleo endelevu ya nchi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam,Katibu huyo Mkuu Mhandisi Said amesema uanzishwaji huo wa Taasisi ya Uongozi umelenga kuhamasisha mabadiliko na ubunifu wa kuendeleza utamaduni wa ushirikishwaji na kuthaminiana.
Akitaja miongoni mwa mafanikio makubwa ya taasisi hiyo ni pamoja na uanzishwaji wa Mtandao wa Wahitimu waliomaliza kozi kutoka katika taasisi hiyo takribani Viongozi 865 wakike na wakiume kutoka sekta mbalimbali,mataifa na tamaduni tofauti.

Mhandisi Said amesema mchanganyiko wa wahitimu hao utaimarisha mitazamo mipya ya kimataifa ,kuchochea ubunifu,uelewa zaidi wa kitamaduni, uthamini wa mitindo tofauti ya uongozi,mabadiliko ya kibinafsi,mabadiliko ya Kazi na Fikra Bunifu.
”Tunapoadhimisha tukio letu la kwanza la wahitimu wa Uongozi leo, nawasihi muikubali maadili ya uongozi wa mabadiliko, na kuwa mabalozi wazuri wa Taasisi.

”Ninaamini kuna fursa kadhaa za nyie kushirikiana na Taasisi,
ikijumuisha kupitia programu za elimu tendaji, midahalo ya sera, na vile vile programu za utafiti na uzalishaji wa maarifa,”amesema.
Amesema Tanzania ilianza mchakato wa uanzishwaji wa Taasisi ya kushughulikia masuala hayo ya Uongozi miaka mingi.”Ilipokuja Mchakato wa Helinski ya kuanzisha kituo cha kikanda cha kukuza uongozi barani Afrika,Tanzania ilikubali Jukumu hilo kwaniaba ya Afrika.

”Serikali ya Finland imekuwa mshirika mkubwa katika safari hii ikitoa msaada muhimu kwa zaidi ya miaka 15,pia msaada wa Umoja wa Ulaya nao umewezesha kupanua kwa kiasi kikubwa mpango wa uongozi kwa wanawake,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo,Kadari Singo amesema kuanzisha kwa Jukwaa hilo la wanajumuiya waliohitimu kozi mbalimbali za Taasisi ya Uongozi kwa lengo la kurudisha kile walichokipata katika taasisi ya Uongozi na kurudisha kwa jamii.
”Kwa jumla waliohudhuria zile programu za muda mrefu hadi sasa ni 860,na leo hapa tumefanikiwa kupata wanajukwaa 400 waliokuja katika uzinduzi huu wa jukwaa.
”Lengo hasa la uwepo wa jukwaa hili ni kuona kwa namna gani wahitimu hao wanaweza kurudisha kile walichokipata kutoka katika Taasisi yetu kwa jamii na kuona wanashirikianaje,”amesema
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Uongozi,Ombeni Sefue amesema mafanikio hayo yote ya Taasisi ya Uongozi yametokana na msaada wa wazi na endelevu kutoka kwa Serikali ya Tanzania na Finland.
”Niwapongeze wakurugenzi wa Bodi waliopita na waliopo sasa,pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Uongozi,Washauri,Wakufunzi na Wadau wa Maendeleo Umoja wa Ulaya,”amesema

More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI