March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

COOP Bank kuzindua huduma mpya kwa wakulima, yadhamini maonesho ya kilimo Dodoma

BENKI ya Ushirika ya COOP Bank imeshiriki kama mmoja wa wadhamini wakuu katika Maonesho ya Kilimo ya Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma wiki hii, na kutumia fursa hiyo kuzindua huduma na bidhaa mpya kwa ajili ya wakulima na vyama vya ushirika.

Akizungumza katika maonesho hayo yaliyoanza leo Agost Mosi 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya COOP Godfrey Ng’ura amesema Bank unaenda  kutambulisha huduma mpya ya Gallapesa, inayowawezesha wakulima kupata fedha kwa kutumia mazao yao kama dhamana kabla ya kuuza kwenye masoko au minada. Aidha, benki hiyo imetangaza huduma ya Cooopesa, inayoruhusu wakulima kufanya miamala kwa njia ya simu, pamoja na mfumo wa Cooney kwa ajili ya vyama vikuu kuchakata malipo kupitia internet banking.

Benki hiyo pia imetangaza huduma ya mawakala wa ushirika, ambapo kwa sasa kuna zaidi ya mawakala 30 nchini, wakihudumia kupitia ofisi za vyama vilivyounganishwa na mfumo wa benki.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, huduma hizo ni sehemu ya mkakati wa kusaidia wakulima kunufaika na mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, na kuwawezesha kupata mitaji kwa wakati kupitia mifumo rasmi ya kifedha. Huduma ya Gallapesa, kwa mfano, hutumia mfumo wa stakabadhi ghalani unaosimamiwa na Mamlaka ya Stakabadhi Ghalani (TMX).

“COOP Bank imekuwa mdau mkubwa wa kilimo nchini, huku asilimia 51 ya umiliki wake ukiwa mikononi mwa wakulima kupitia vyama vya ushirika. Benki hiyo inahudumia mazao yote ya kimkakati kama vile kahawa, korosho, chai, ufuta, mbaazi na pamba, kupitia usimamizi wa vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu.”amesema

Tangu kuanzishwa kwake rasmi mwezi Oktoba 2024, COOP Bank imefungua matawi katika mikoa ya Kilimanjaro (Moshi), Mtwara (Tandahimba), Tabora, na Dodoma, ambako pia ndiko yalipo Makao Makuu yake.

Ametoa wito kwa wakulima, vyama vya ushirika, vijana, na wafanyabiashara wanaoshiriki katika mnyororo wa mazao ya kilimo kutembelea banda hilo ili kupata elimu juu ya huduma zinazotolewa.

Aidha, hadi kufikia Julai 2025, COOP Bank ilikuwa imepitisha zaidi ya shilingi bilioni 150 kwa ajili ya malipo ya wakulima wa mazao ya ufuta, mbaazi na korosho katika mikoa ya Songwe, Songea, Mtwara na Lindi kupitia mfumo wa internet banking uliounganishwa na vyama husika.