March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sekondari ya Kazima yaboresha miundombinu kwa ajili ya wenye ulemavu

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online -Tabora

Serikali imepeleka zaidi ya milioni 160 shule ya sekondari Kazima iliyoko mkoani Tabora ili kuboresha miundombinu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.

Akizungumza na Majira Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Tabora,Dkt.John Pima, amesema kiasi hicho cha fedha kimetumika kujenga miundombinu rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika shule hiyo.

Amefafanua kuwa shule hiyo ambayo ni jumuishi ina jumla ya wanafunzi 1002 wakiwemo watoto wenye mahitaji maalumu wa kike na kiume 135, wasio na mahitaji maalumu wakiwa 867 kwa kidato cha kwanza hadi cha sita.

‘Fedha hizi zimetumika kujenga vyumba 4 vya madarasa ya kisasa kwa watoto wenye mahitaji maalumu, ofisi 6 na vyumba 2 vya upimaji matamshi na usikivu kwa watoto wenye usikivu hafifu ili waweze kusoma vizuri darasani’, amesema.

Dkt.Pima amebainisha kuwa watoto hao walikuwa wanashindwa kufanya vizuri katika masomo yao kutokana na changamoto ya miundombinu, hivyo kujengwa miundombinu hiyo kutawarahisishia kusoma vizuri na kupata elimu bora.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Dafroza Mwampondele, ameishukuru Serikali kwa kujali na kutambua umuhimu wa kundi hilo la wanafunzi na kuwatengea bajeti,ili kuboresha mazingira ya shule na miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji iwe rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu shuleni hapo.

Hata hivyo Mwenge wa Uhuru mwaka huu ukiwa katika Halmashauri hiy ulitembelea, kukagua na kuzindua ujenzi wa miundombinu hiyo ambapo Kiongozi wa Mbio hizo Ismail Al Uss,amesema,utekelezwa miradi hiyo kunatokana na dhamira ya dhati ya Rais ya kuona watoto wenye mahitaji maalumu nchini wanapatiwa elimu na miundombinu ya shule zao inakuwa rafiki ili isiwe kikwazo cha kupata elimu bora.