Na Israel Mwaisaka,Timesmajira Online -Rukwa
Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) yaliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa,yameshauriwa kuongeza juhudi katika kuchochea maendeleo ya jamii badala ya kusubiri utekelezaji kutoka kwa Serikali pekee.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga,Nyakia Chirukile, wakati akifungua kongamano la NGO’s lililowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mafanikio ya sekta hiyo katika nyanja mbalimbali nchini.

Chirukile amesisitiza kuwa mashirika hayo yanapaswa kuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii kuhusu maadili mema, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, uhifadhi wa mazingira pamoja na kuhamasisha usafi wa mazingira ili kuijenga jamii yenye ustawi wa kijamii na kiuchumi.
“NGO’s zina mchango katika maendeleo ya taifa,ni muhimu ziendelee kushirikiana na Serikali kuibua na kutatua changamoto zinazokabili wananchi.Ninyi ni wadau wa maendeleo toeni elimu kwa jamii kuhusu uadilifu na kukemea tabia ovu katika jamii,” amesema Chirukile.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Pendo Mangali,amewataka washiriki hao kutoka mashirika mbalimbali kufanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wao, baadhi ya wawakilishi wa Mashirika hayo walioshiriki kongamano hilo wamepongeza hatua ya Serikali ya kuweka mazingira bora ya taasisi hizo kufanya kazi mbalimbali za maendeleo kwa usatawi wa jamii.

Mkutano huo umeimarisha mshikamano kati yao na Serikali huku wakiahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
“Tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kuondokana na changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili jamii katika kufanikisha maendeleo,”.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi