March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chatanda awaasa Wajumbe Mkutano Mkuu Maalum   UWT kujiepusha na rushwa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MWENYEKITI  wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Mariam Chatanda, amewaonya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa UWT dhidi ya vitendo vya rushwa katika  uchaguzi wa kuwapata wawakilishi wa Viti Maalum Bungeni huku akisistiza kuchaguliwa kwa watu wenye uwezonwa kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi badala ya kushawishiwa kwa fedha.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika kesho Julai 2, 2025 jijini Dodoma, ukihusisha uchaguzi wa wabunge wa Viti Maalum kupitia makundi maalum, yakiwemo ya Asasi za Kiraia (NGOs), wafanyakazi, wasomi wa vyuo vikuu, na watu wenye ulemavu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 1, 2025 ofisini kwake jijini Dodoma, Chatanda alisema”Tunaelewa wagombea na wapambe wao wameshafika Dodoma kwa ajili ya Mkutano wetu wa kesho,nawaomba wajumbe wote wachague wawakilishi kwa kuzingatia uwezo wao wa kazi, si kwa kuwapa rushwa.”

Aidha, amewataka wajumbe wote kutoka maeneo mbalimbali nchini kuzingatia maadili ya uchaguzi huo na kuwakaribisha rasmi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi wa wawakilishi wa makundi hayo kwenda Bungeni kupitia UWT.

Chatanda pia amewahimiza wanawake waliochaguliwa katika ngazi ya mikoa kwa ajili ya Ubunge na Udiwani wa Viti Maalum, pamoja na wanachama wengine wa CCM, kuongeza juhudi za kufanya kampeni ili kuhakikisha ushindi wa chama katika Uchaguzi Mkuu ujao ili kupata mgao wa viti vingi Bungeni.

“Lazima wafanye kampeni za Rais, Wabunge na Madiwani. Ushindi mkubwa wa CCM kwenye uchaguzi mkuu ndio utakaowezesha kupatikana kwa Viti Maalum vingi kupitia chama,” alisisitiza.

Hata hivyo, Chatanda alikumbusha kuwa ushindi katika kura za mikoa hauhitimishi safari ya kupata nafasi ya uwakilishi, kwani uteuzi wa mwisho hufanywa kupitia vikao vya juu vya chama baada ya mchujo wa kina.

“Ushindi wa kura siyo uteuzi. Bado kuna vikao vya mchujo hadi CCM itakapopitisha majina rasmi ya wagombea wa Ubunge na udiwani wa Viti Maalum,” amesema.

Amewataka wanachama kutojisahau au kubweteka, bali waendelee na kampeni kwa nguvu zote ili CCM ipate kura nyingi zitakazoliwezesha kushinda nafasi nyingi za uwakilishi, zikiwemo za Viti Maalum.