March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UVCCM Taifa kufanya  Mkutano Mkuu Maalum wa kihistoria Jijini Dodoma

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma

JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imeingia katika hatua za mwisho za maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum unaotarajiwa kufanyika kesho, Agosti 1, 2025, jijini Dodoma, kwa ajili ya kuchagua vijana watakaoiwakilisha Jumuiya hiyo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la Wawakilishi kupitia kundi la vijana.

Akizungumza leo Julai 31,2025 na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM Taifa,  Jesca Mshama, amesema kuwa mkutano huo ni wa kihistoria na unaandaliwa kwa kiwango cha juu ili kuenzi heshima ya Jumuiya ya Vijana, Chama, naRais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwa ajili ya vijana wa Tanzania.

 “Mkutano huu ni wa kihistoria. nadhani mmeona wenyewe jinsi maandalizi yalivyo makubwa na mazuri,tunataka kuonesha heshima yetu kwa Jumuiya, kwa Chama, na hasa kwa Rais wetu Dkt. Samia ambaye amekuwa mtetezi wa kweli wa vijana,” amesema Jesca Mshama.

Mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe takribani 438 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, na unatarajiwa kutoa fursa kwa vijana kuchagua wawakilishi wao wanaoaminiwa kuwa wataendelea kusimamia kwa dhati maslahi ya vijana ndani ya vyombo vya maamuzi.

 “Wale tunaowachagua kesho ni vijana waliopikwa na chama hiki kikongwe, tuna imani kuwa watakwenda kuwakilisha sauti na matumaini ya vijana wa Tanzania,” ameongeza Mshama.