Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametoa wito kwa wananchi wote nchini, kuwa waangalifu na kujiepusha na baadhi ya watu wasiojulikana ambao wamekuwa wakifanya udanganyifu katika mitandao na kuzua taharuki.
Katika taarifa iliyotolewa Julai 21, 2025 na Kaimu Katibu wa Habari wa Katibu Mkuu wa CCM, Aboubakary Liongo, imedai kuwa, hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la matukio ya udanganyifu yanayofanywa na watu wasiojulikana wakitumia jina la Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa chama hicho kwa lengo la kuwatapeli wananchi kupitia barua pepe,ujumbe mfupi(sms) na mitandao ya kijamii.

Ameelezea moja ya mfano wa udanganyifu huo kuwa ni pamoja na barua pepe inayodaiwa kutumwa na ‘EMMANUEL NCHIMBI’ kupitia anwani ya barua pepe nchimbiemmanuel16@gmail.com, ikidai kuwepo kwa taarifa muhimu zinazohitajika kutoka kwa mpokeaji.
Hivyo,umma umetaarifiwa kuwa, ujumbe huo si halali na hauhusiani kwa namna yoyote na Katibu Mkuu huyo wa CCM wala taasisi yoyote rasmi ya chama na Serikali.
Huku akisisitiza kuwa, Balozi Nchimbi hatumii barua pepe binafsi katika masuala ya kitaasisi au chama wala viongozi wa chama hicho au Serikali kutotumia ujumbe wa siri kwa masuala ya kikazi kupitia barua pepe binafsi au njia zisizo rasmi kama hizo.
Aidha wananchi wametakiwa kuripoti katika vyombo vya usalama au kwa uongozi wa CCM katika ngazi husika, endapo watapokea ujumbe wa kutia shaka.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi