Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online -Rukwa
WASIMAMIZI wa uchaguzi ngazi ya mikoa na majimbo wa mikoa ya Rukwa na Katavi wameaswa kusoma na kuelewa kwa kina katiba,sheria,kanuni,taratibu na miongozo mbalimbali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuandaa na kufanikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Magdalena Rwebangira,akifungua mafunzo kwa waratibu,wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ndani ya majimbo hayo.

Mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwawezesha wasimamizi hao kuwajibika kikamilifu na kwa weledi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Magdalena, amesisitiza kuwa uchaguzi ni mchakato na wenye changamoto nyingi, hivyo ni muhimu kufuata katiba,sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa pamoja na kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vilivyo sajiliwa katika hatua zote za uchaguzi kwa kuzingatia matakwa ya kikatiba na sheria.
Pia amesema,wasimamizi hao wanapaswa kujiepusha kuwa chanzo cha migogoro na malalamiko yanayotokana na vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi,hivyo wanatakiwa kuhakikisha wadau wote wanashirikishwa kama ilivyoainishwa katika miongozo mbalimbali ya tume hiyo ili kufanikisha mchakato mzima kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi, Saida Hillary,amesema mafunzo hayo yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini, yanalenga kuwajengea uwezo wasimamizi wa uchaguzi katika kutekeleza majukumu yao kama inavyoelekezwa kisheria na na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Saida,amewasisitiza wasimamizi wote kutumia ujuzi na uzoefu kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakwenda vyema bila matatizo, na kwamba tume haitamvumilia mtendaji yeyote anayezalisha matatizo au malalamiko ambayo yataathiri mchakato mzima wa uchaguzi.
Wasimamizi hao pamoja na watendaji wote wanaohusika na uchaguzi wamekula kiapo cha kutunza siri na kujitoa uanachama wa vyama vya siasa mbele ya Hakimu mkazi Mwandamizi wa wilaya ya sumbawanga Lilian Moses Ndelwa

More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI