March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni ya Chuma kwa Chuma Sio Poa yazinduliwa

Na Mwanidishi Wetu,Timesmajira Online

KAMPENI ya Kitaifa ya uhamasishaji wa usalama barabarani ijulikanayo kama,“Chuma kwa Chuma Sio Poa”,imezinduliwa kwa lengo la kuwahamasisha waendesha bodaboda na bajaji kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Kampeni hiyo imezinduliwa na Kampuni ya Oryx Energies Tanzania Limited,ikienda sambamba na kukabidhi vibanda vya kisasa kwa ajili ya kumpuzika askari wanapokuwa barabarani wakitekeleza majukumu yao.

Akizungumza Julai 19,2025,jijini Dar-es-Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi(IGP) Camilius Wambura, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi ,Kikosi cha Usalama Barabarani ACP. Joseph Mwakabonga, amesema kampeni hiyo itasaidia kuwajengea uelewa zaidi madereva bodaboda na bajaji kuzingatia sheria za usalama barabarani.

“Kampeni hii ya Oryx Energies ya kutoa elimu ya usalama barabarani kwa bodaboda ni suala mtambuka,ambalo kila mtu ambaye ni Mtanzania anatakiwa kuwa sehemu ya kufanikisha kampeni hii ,tunawapongeza kwa kuona umuhimu wa kuwapa elimu hii ndugu zetu wa bodaboda na bajaji,”.

ACP Mwakabonga, amesema kampeni hiyo itawafanya waendesha pikipiki na bajaji kuachana na tabia ya kutofuata sheria za usalama barabarani ,hivyo imani yao watumiaji wa vyombo hivyo watazingatia sheria na hatimaye kupunguza au kumaliza ajali zinazotokana na vyombo hivyo vya moto.

Amesema,suala la barabarani bado imekuwa changamoto nchini, hivyo uwepo wa wadau ambao wanaona muhimu wa kutoa elimu ya usalama barabarani ni jambo la kupongeza na kuungwa mkono.

Pia amesema,vibanda vya kisasa ambavyo wamekabidhiwa na kampuni hiyo,vitawasaidia askari wa kikosi cha Usalama Barabarani kutekeleza majukumu yao wakati wote kwani vimefunfwa mfumo wa taa za nishati ya jua(sola).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania, Imani Mtafya, amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko chanya kwa waendesha pikipiki na bajaji pamoja na watoa huduma wengine kuhusu usalama barabarani.

Amesema,malengo ya kampeni hiyo ni pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendeshaji bodaboda na bajaji kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi,kutoa michango ya vitendea kazi kama vibanda vya kisasa vya askari vinavyotumia nishati ya jua, kofia ngumu, jaketi za kuonekana usiku, vizima moto pamoja na vilainishi bora vya mitambo, pikipiki na magari.

Amesema,kupitia kampeni hiyo wamefanikiwa kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa wasafirishaji zaidi ya 200 kwa kila wilaya za Mkoa wa Dar-es-Salaam, huku ikilenga kupanua mafunzo hayo nchini kote.

Sanjari na hayo awewataka waendesha vyombo hivyo vya moto kutumia fursa ya kampeni hiyo kuwa mabalozi kwa wenzao huku akivisisitiza vyombo vya habari umuhimu wa kueneza ujumbe huo,ili kuhakikisha jamii nzima inashiriki katika kuzuia ajali kwani “Ajali nyingi zinaweza kuzuilika. Elimu na uwajibikaji ni silaha kubwa zaidi”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Oryx Gas Tanzania Ltd ambayo ni moja kati ya kampuni zilizopo chini Oryx Energies,Benoit Araman,amesema kampeni hiyo inalenga kuelimisha na kuhamasisha usalama wa barabarani, hasa kwa waendeshaji wa pikipiki na bajaji, ambao ni sehemu muhimu ya usafiri wa kila siku.

“Tunaamini kwa pamoja tunaweza kupunguza ajali, kulinda maisha, kutumia nishati safi na kusaidia uchumi na maendeleo ya taifa letu,”amesema Araman.

Awali Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar-es-Salaam na Taifa Said Chega,amesema ni muhimu kuendelea kupata elimu ya usalama barabarani na kusisitiza kupitia kampeni ya Chuma kwa Chuma Sio Poa,watapunguza ajali za barabarani kwani watakuwa wanakumbushwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

“Kila siku katika shughuli zetu tunapokea madereva wapya,wapo wa elimu ya msingi na sekondari ambao wanakuja kuungana nasi, hivyo kunapokuwa na mafunzo ya aina hii yanasaidia kutujengea uelewa na kuchukua tahadhari kwa kuheshimu sheria za usalama barabarani.

Amesisitiza kuwa kuna haja ya waendesha pikipiki kuendelea kupatiwa elimu kwani ndio wanasafirisha abiria kila siku hivyo wanapokuwa na elimu hiyo maana hata abiria nao wanakuwa salama.