Ashura Jumapili, Timesmajira Online-Bukoba
Kiasi cha bilioni 9 zinatarajiwa kutumika kujenga jengo la kisasa la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera,ambalo litakuwa na ukumbi wenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 350.
Hayo yamesema na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya eneo la mradi kwa mkandarasi,ambapo amesema ofisi ya sasa ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ina miaka zaidi ya 60 na ubora wake umepungua kwa kiasi kikubwa.

“Ofisi hii iliwahi kupitiwa na tetemeko,ziwa linaendelea kusogea na nyumba nyingi za watumishi zimemezwa na maji,hivyo kuendelea kuboresha jengo hilo ni kupoteza fedha za serikali,mchakato ulikuwa mrefu hadi kufikia hatua ya kumkabidhi mkandarasi kazi haikuwa rahisi,”amesema Hajat Mwassa.
Amesema mkandarasi ameshalipwa asilimia 25 ya fedha kati ya shilingi bilioni 4.6 za mradi wa ujenzi wa jengo hilo awamu ya kwanza.Huku akisisitiza kuwa Kagera inakwenda kuwa miongoni mwa Mikoa ya kisasa na kuwa sehemu ya kivutio kwa wageni.
Awali Mhandisi Raphael Nyatega kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ,amesema mradi huo wa ujenzi umeanza mwaka wa fedha 2024/2025 na unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2025/2026.
Mhandisi Nyatega amesema hatua ya awali ilikuwa kufanya maandalizi ya mradi kulingana na mahitaji ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kazi hiyo imefanyika na wataalam kutoka hiyo kwa kushirikiana na Mhandisi Mshauri Elekezi.
Amesema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu mbili na awamu ya kwanza itakuwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wasaidizi wake, Katibu Tawala wa Mkoa na wasaidizi wake,ukumbi wa mikutano utakao kuwa na uwezo wakubeba watu 350,mgahawa mkubwa wa kisasa,ofisi ya habari maelezo na ofisi ya uwekezaji.
“Awamu hiyo pia itajumuisha ujenzi wa uzio,nyumba ya walinzi na ofisi ya madereva”anasema Mhandisi Nyatega.

Pia amesema usanifu wa jengo hilo umezingatia nafasi ya Mkoa kimkakati katika uwekezaji,ambapo awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo umesainiwa mkataba wa bilioni 4.6 na utakamilika kwa muda wa miezi 12 na mkandarasi huyo anasimamiwa na Mshauri Elekezi.
Huku awamu ya pili itakuwa ujenzi wa jengo la watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa,wakuu wa sehemu,vitengo pamoja na maofisa wote na wasaidizi wa ofisi.
Hivyo amesema,awamu hiyo ipo katika hatua za usanifu inatarajiwa kugharimu kiasi cha bilioni 4.4,hivyo kufanya jumla ya bilioni 9, kukamilisha mradi huo.
Huku akitaka faida za mradi huo kuwa ni pamoja na kuboresha utoaji huduma kwa Wananchi katika njia za haraka na za kisasa na mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi.Pia mradi utaweka mfumo wa vitendea kazi wa kisasa ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia,kuwa na eneo la kimkakati la kukaribisha na kuvutia wawekezaji na kuboresha mandhari ya mji wa Bukoba.
Naye Mhandisi Mshauri Mwelekezi wa mradi huo,Mbunifu Majengo ( Architect ),Gozbert Kakiziba, kutoka kampuni ya ( GOZTECTURE GROUP LTD),amesema jengo litakuwa imara halitapata shida ya kupitiwa na tetemeko na litakaa zaidi ya 100.

Kakiziba,amesema,mkandarasi apaswi kufanya chochote bila idhini ya Mshauri elekezi huku akisisitiza kuwa sampo zote zipimwe kabla ya kutumika ili pande zote mbili ziwe salama pamoja na kutoa ripoti kila mwezi ya maendeleo ya ujenzi.
Amemtaka pia mkandarasi huyo kutumia vibarua wanaotoka eneo la mradi hasa kuwazingatia wanawake na watu wenye ulemavu kwa shughuli wanazoweza kufanya.
Mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo ni Haamid Ashraf kutoka kampuni ya ( Skywords Construction Co.ltd )


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi