March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania watakiwa kuombea uchaguzi ufanyike kwa amani na kujitokeza kupiga kura

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Wito umetolewa kwa Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kuombea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu pamoja na kushiriki kupiga kura kuchagua viongozi,ili kukua kiroho na kuchochea maendeleo ya  nchi.

Hayo yameelezwa Juni 28,2025 na Kiongozi wa huduma ya uamusho Afrika Mashariki na Kati, Askofu Timoth Paulo,katika kongamano linaludumu kwa muda wa siku sita mkoani Mwanza la maombi ya uamsho lililowakutanisha watu kutoka nchi za Afrika Mashariki,huku ujumbe uliotawala  ni kuombea wenye mamlaka kufanya maamuzi sahihi pamoja na kuombea amani na  uchaguzi.

“Kila mmoja kwa imani yake aombe amani ya nchi,aombee uchaguzi uwe wa haki,huru, uishe salama bila vurugu zozote  na bila watu kumwaga damu,kupigana wala kuwa na visasi,”amesema Askofu Timoth.

Askofu Timoth,amesisita Watanzania wenye sifa kila mmoja kushiriki katika uchaguzi kwa kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowakilisha changamoto za wananchi na kuwaletea maendeleo.

“Katika kukua kiroho na maendeleo ya nchi ,ni muhimu kila mwananchi kushiriki katika uchaguzi na kupiga kura, kwani yeye ndio anaye mchagua mwakilishi wake.Mwakilishi uliye mchagua ndiye anaenda kumsemea yeye ili kumletea maendeleo,hivyo tunakuwa na serikali nzuri,Bunge na Madiwani na viongozi wazuri wa vitongoji na mitaa ikiwa sisi wenyewe tumewajibika kuwachagua,”.

Pia amesema,kupitia kongamano hilo wamefundishana umuhimu wa kuombea viongozi wa Serikali na Wakuu kama maandiko matakatifu yanavyosema kuwa “kabla ya mambo yote tunatakiwa kuombea watu wote,tuombee amani,wenye mamlaka na wafalme ili wote tuishi kwa amani,”.Ili wenye mamlaka watawale kwa haki na uzuri kwa faida ya jamii na watu wanaowaongoza.

Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo akiwemo akiwemo,Naibu Askofu Mkuu Patricia Kimonge,wa huduma ya toba na utakatifu Tanzania,amesema,maombi hayo ni kwa ajili ya kusaidia kanisa na taifa kusimama katika nafasi yake.

“Mbele yetu tuna uchaguzi ambao ni wakati nyeti kama Tanzania tulionao,tunahitaji kama wakristu tuweze kusimama na kulibeba taifa letu katika toba na maombi ili yale yote ambayo ni makusudi ya adui juu ya taifa hili hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi,Mungu wetu aweze kutuvusha salama,”amesema.

Muimbaji kutoka Njombe nchini Tanzania Debora Lameck,amesema,”Watanzania tunapaswa kuliombea taifa letu,na siyo viongozi pekee waliopo madarakani na kwenye vyama vya siasa wanaweza kuleta amani,kama kanisa tuamke sasa kuliombea taifa amani,wakati wa kampeni na uchaguzi ili tuvuke salama bila machafuko,”.

Naye Mhubiri wa kanisa la Methodiste Libri Bunjumbura nchini Burundi,Saidi Nzohabonayo,amesema,uchaguzi mzuri unapitia kwa watu kumuomba Mungu kwani bila hivyo hawawezi kupata watu sahihi.

Mchungaji Athanase Badahakane kutoka kanisa la on the Rock nchini Rwanda,amesisitiza kuwa kabla ya kupiga kura wananchi wanapaswa kumuomba Mungu ili awapatie mtu sahihi.Huku akisema kongamano hilo linasaidia  kuleta umoja na kusaidia kugombea viongozi wa nchi hizo kuwa na amani na kuondoa machafuko.