March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Msichana Initiative yazindua programu ya Sauti Yetu,Nguvu Yetu awamu ya pili

Na Penina Malundo,Timesmajira

TAASISI ya Msichana Initiative imezindua programu ya Sauti Yetu,Nguvu Yetu kwa awamu ya pili ambayo inawashirikisha wasichana 20 kutoka mikoa minne ikiwemo Dar es Salaam,Pwani,Tabora na Dodoma.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi wa Taasisi hiyo,Rebecca Gyumi wakati wa uzinduzi wa Programu hiyo kwa awamu ya pili alisema programu hiyo ni ya miaka miwili ambayo inawaunganisha kwa pamoja wasichana kujenga nguvu za pamoja na kuleta sauti yao kwenye masuala muhimu kuwawezesha kupata haki zao kama wasichana katika taifa.

Amesema hii ni awamu ya pili ya mafanikio waliyoyaona katika programu hiyo kwa awamu ya kwanza ambapo wasichana vinara 20 waliweza kuwafikia na wao kuwa vinara katika kuwafikia wasichana wengine 240 kutoka katika maeneo yao.

”Awamu ya kwanza ya programu yetu imeweza kupiga hatua kubwa kwani tumeona hawa wasichana 20 waliomaliza awamu ya kwanza,baadhi yao kuanza kuonesha nia na kudhubutu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa mwaka huu ikiwemo wengine kwenda katika viti maalum na majukwaa ya wanawake kwenye maeneo yao.

”Nawengine kuonesha nia moja kwa moja katika uchaguzi wa mwaka huu kwenda kuchukua fomu ya kugombea nafasi mbalimbali za udiwani,haya ni mafanikio makubwa kuona namna wasichana hawa walivyokuwa wanajiamini na kusimama katika majukwaa katika kujiongelea,”amesema

Amesema wasichana wanapopata majukwaa sahihi ya kuongelea mambo yao inaonesha nguvu ya kuona kwamba hayupo pekee yake bali kuna wasichana wengine kama yeye wanaopitia mambo mbalimbali ambapo wanaweza kuonesha nguvu yao ya kutoa hofu kwani wasichana wanauwezo mkubwa na hawahitaji kuzungumziwa wanaweza kujizungumzia kwani wanafahamu matatizo yao wanayopitia.

”Tunashukuru kuona programu hii inazidi kuleta mafanikio makubwa kwa jamii ambapo awamu ya pili nayo imechukua wasichana 20 wanaotoka katika mikoa mbalimabali ambayo wamekuwa wakifanya nayo kazi na hii yote ni kuonesha bado wasichana wanahitaji kupewe nyenzo na rasilimali za kujisimamia wao wenyewe,” amesema .

Mmoja wa Wasichana Vinara walioshiriki Programu hiyo awamu ya kwanza kutoka Mkoa wa Tabora Wilaya ya Nzega,Loveness Athumani amesema programu hiyo ya sauti yetu, nguvu yetu imewasaidia wao kujitambua,kujiamini na kutambua haki zao ambazo hawakuwa hawazijui toka mwanzo.

”Jamii ya Wakulima na Wafugaji,wanaamini mtoto wa kike kazi yake ni kuolewa na hamna kitu kingine,programu hii imewafungulia kwamba msichana anahaki yakufanya kila kitu ikiwemo haki ya kusoma,kushiriki na kushirikishwa,haki ya kuamua yeye mwenyewe anachotaka,”amesema.

Amesisitiza kuwa programu hiyo ilikuwa inaagenda nyingi ikiwemo agenda ya uongozi ambapo imemfunguli yeye njia ya kuwa kiongozi kwa sababu anauwezo wa kujiamini na kujitambua.

Leonardina Sosthenes Msichana Kinara kutoka Bagamoyo,amesema kutokana na mafunzo aliyoyapata awamu ya kwanza ya programu hiyo yamemsaidia kuwa na nguvu na kuzidi kujiamini katika kujisimamia.

”Zamani tulikuwa hatuwezi kuongea kutokana na hofu tuliyokuwa tumejengewa tangu tulipozaliwa kuwa mtoto wa kike ni lazima kushuka chini na hatuwezi kuongea hata kama sehemu ni haki yako.

”Mafunzo niliyopata ndani ya miaka miwili yamenijenga kuweza kusimama sehemu yoyote na kuongelea kitu ambacho ni haki yangu na haki ya msichana,”amesema.

Dafrosa Dickson Msichana Kinara Mkoa wa Dar es Salaam mshiriki awamu ya Pili ya Programu hiyo,amesema taarifa ya mradi huo aliona kwa njia ya mtandao wa kijamii na kuweza kuchaguliwa kushiriki katika programu hiyo ya miaka miwili.