March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAMISEMI yashauriwa kuziagiza Halmashauri kupeleka walimu kusoma ADEM

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online , Dodoma

WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Tanzania (ADEM) imetoa rai kwa Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuzitaka halmashauri kote nchini kuweka mkakati wa kupeleka walimu kusoma katika taasisi hiyo, ili kuinua ubora wa elimu kupitia usimamizi na uongozi bora.

Akizungumza jijini Dodoma Juni 19,2025 katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Afisa Utumishi Mkuu wa ADEM, Waziri Mohamed Waziri, amesema hatua hiyo inaenda kuleta ubora wa elimu nchini.

Amesema,Taasisi hiyo inaendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu yanayolenga kuwajengea uwezo walimu katika usimamizi na uongozi wa elimu pamoja na udhibiti ubora wa elimu katika shule za msingi na sekondari.

“Lengo kuu la kuanzishwa kwa ADEM ni kuwafikia walimu wote nchini, ili kuwajengea weledi wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuhakikisha elimu inayotolewa nchini ni bora na si bora elimu,” alisema Waziri.

Ameeleza kuwa mafunzo ya muda mrefu yanayotolewa ni pamoja na stashahada ya Udhibiti Ubora wa Shule na Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa kwa walimu waliopitia ADEM katika kuboresha utendaji kazi wao.

Kwa mujibu wa Waziri, tafiti zinaonesha kuwa walimu waliopata mafunzo kutoka ADEM wamekuwa na ufanisi mkubwa katika kusimamia elimu katika maeneo yao ya kazi, hivyo kuna haja ya halmashauri zote kuangalia umuhimu wa kuwapeleka walimu wao katika chuo hicho.

“Tunaiomba TAMISEMI kuzielekeza halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya mafunzo haya na ikiwezekana kuwe na mpango mahsusi wa kuhakikisha kila mwaka halmashauri zinapeleka walimu wachache ADEM,hii itatujengea msingi imara wa uongozi bora wa elimu katika ngazi zote,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkutubi wa ADEM, Sarah Emmanuel, amebainisha kuwa matokeo chanya yameonekana kwa walimu waliopitia mafunzo ya ADEM, hususan katika kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika shule walizorejea.

“Mwalimu aliyepitia ADEM anakuwa na mtazamo mpya juu ya majukumu yake ya kila siku. Anafahamu vigezo vya msingi vya elimu bora na anakuwa tayari kusimamia mabadiliko katika mazingira ya shule,” amesema.

Naye Karimu Msafiri Kiungandua, mmoja wa viongozi wa ADEM, amesema chuo hicho kwa sasa kiko katika kipindi cha udahili kwa ajili ya kozi zake mbili kuu ambazo ni Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu pamoja na Stashahada ya Udhibiti Ubora wa Shule, huku pia wakitoa nafasi za masomo kwa njia ya masafa kwa walimu wasioweza kupata likizo ya kusoma.

“Tunawakumbusha walimu wote nchini kuwa ADEM ni sehemu sahihi ya kuwajengea maarifa ya msingi katika kusimamia elimu. Mafunzo haya ni dira ya mabadiliko ya kweli katika sekta ya elimu ya Tanzania,” amesema Kiungandua.

Kwa ujumla, ADEM inatoa mwaliko wazi kwa walimu wote na watoa maamuzi katika sekta ya elimu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwajengea walimu uwezo wa kiuongozi na kitaaluma, kama njia mojawapo ya kuboresha mfumo mzima wa elimu nchini.