March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RAS Dar ataka watafiti kuibua mbinu mpya tiba ya Selimundu

Na Heri Shaaban,Timesmajiraonline,Dar

KATIBU Tawala Mkoa Dar es Salaam,Toba Nguvila,ameshauri watafiti kutoka taasisi mbalimbali nchini kuendelea kufanya tafiti juu ya ugonjwa wa selimundu ili kuibua mbinu mpya za tiba, kinga na uboreshaji wa huduma juu ya ugonjwa huo.

Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha zaidi ya Watoto 300,000 uzaliwa na Sikoseli kila mwaka Duniani na hapa nchini takribani watoto 14,000 uzaliwa na ugonjwa huo

Nguvila,amesema hayo jijini hapa leo Juni 19,2025 katika maadhimisho ya siku ya Selimundu Duniani ambapo Kitaifa imefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana wilayani Ilala.

“Watoto 14,000 uzaliwa na ugonjwa wa Sikoseli nchini nchi yetu ni ya nne Duniani kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa sikoseli nyuma ya Nigeria,India,na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo nchi yetu inakadiriwa kuwa na zaidi ya wagonjwa 200,000 wa Sikoseli”amesema  Nguvila.

Katibu Tawala Nguvila amesema watoto saba kati ya watoto 100 wenye umri wa kati ya miaka mitano hufariki kutokana na madhara ya ugonjwa huo.

Aidha Toba Nguvila,amesema Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutekeleza sera ya afya ya mwaka 2007 kwa kuimarisha huduma dhidi ya magonjwa yasioambukiza ikiwemo Selimundu,huduma zimeboreshwa kupitia upatikanaji wa vipimo mapema na dawa na vifaa.

Hivyo ametoa wito kwa watafiti na taasisi za umma za tiba Mbadala na tiba Asili kuendelea kufanya utafiti juu ya ugonjwa huo  wa Selimundu ili kuibua mbinu mpya za tiba,kinga na huboreshaji wa huduma.

Aliongeza kuwa ushirikiano wa Kimataifa unaitajika katika juhudi za ugonjwa huo kwa kuwa ugonjwa wa Selimundu hauna mipaka kijiografia  kauli mbiu ya mwaka huu 2025 inasema “Hatua madhubuti za Kitaifa kwa matokeo chanya ya kijamii kuwezesha Jamii kutambua ,kuzuia na kukabiliana na Selimindu “

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana Brayson Kiweli,amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana ina Kliniki ya ugonjwa wa Sikoseli ina zaidi ya miaka 17 na inatoa huduma zake kila siku mpaka sasa katika hospitali hiyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi,Mama na Mtoto Dkt.Ahmad Mohamed ,amesema  kila Mtoto anayezaliwa na Sikoseli anayo haki ya kuishi Serikali na vituo vya kutoa huduma vinaendelea kutoa huduma nchini kwa ajili ya wagonjwa wa Selimindu.