BRELA Yasogeza Huduma kwa Wananchi Kupitia Maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
Na Joyce Kasiki, Dodoma
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wamejumuika kwenye maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa ili kurahisisha usajili na upatikanaji wa leseni.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 16,2025 katika viwanja vya maoneyesho hayo Chinangali Park jijini Dodoma,Afisa Leseni Mwandamizi wa BRELA, Koyan Abubakari, alisema kuwa wanatoa huduma zote muhimu moja kwa moja kwenye banda lao, ikiwemo usajili wa biashara, usajili wa viwanda, na utoaji wa leseni za Biashara Kundi A zenye sura ya kitaifa au kimataifa.
“Tunatoa huduma za leseni za viwanda kwa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vinavyosimamiwa na BRELA. Pia tunatoa usajili wa biashara kwa mtu mmoja hadi kikundi cha watu 20; wakizidi hapo, wanashauriwa kusajili kampuni,” alisema Abubakari.
Kwa mujibu wa Abubakari , mteja anayetaka kusajili jina la biashara anapaswa kuwa na taarifa kamili zikiwemo Namba ya NIDA, namba ya simu, barua pepe hai pamoja na TIN ya mmiliki. Umri wa mteja haupaswi kuwa chini ya miaka 18.
Huduma zote zinapatikana papo hapo kwa yeyote atakayefika na nyaraka sahihi, na zinatolewa bure bila ada yoyote kama sehemu ya maadhimisho hayo ya kitaifa yanayolenga kumuwezesha mwananchi.
Abubakari aliongeza kuwa ushiriki wa BRELA katika maonyesho haya ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kusajili biashara zao kisheria ili kupata fursa mbalimbali za kiuchumi na kisheria.
Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani kufika katika banda la BRELA ili kupata huduma hizo muhimu ambazo ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kitaasisi nchini.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani