Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline, Kilindi
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi amesema ana matumani makubwa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwa watakamilisha Mradi wa Maji Kwamaligwa- Gitu kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Akizungumza Juni 7, 2025 mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Kwamaligwa- Gitu, uliopo Kijiji cha Kwamaligwa, Kata ya Kibirashi, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, amesema mradi huo ni muhimu kukamilika sababu unategemewa na wananchi wa vijiji saba vyenye wananchi 36,263.
“Nataka kuwaambia ndugu wananchi, mradi huu kwa vile Mwenge wa Uhuru umefika hapa siku ya leo, unakwenda kukamilika muda si mrefu kwa asilimia 100, na tutaongoza kwa kupata maji safi na salama, na tutasahau kabisa kama sisi wananchi wa maeneo haya tuliwahi kupata changamoto ya maji.

“Hivyo nawaahidi kupitia Mwenge wa Uhuru kuwa maji yatapatikana kwa sababu wenzetu wa RUWASA wamejipanga kikamilifu, fedha zipo, na wapo tayari kutekeleza mradi huu kwa kumuwekea heshima Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Ussi.
Naye Diwani wa Kata ya Kibirashi Bakari Fau alisema kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha vijiji vya Kwamaligwa, Kibirashi, Gombero, Koa, Gombero Madukani. Lakini mradi huo pia utasambaza maji vijiji vya Elerai na Gitu. Vijiji vya Elerai na Gitu ndiyo vilikuwa na changamoto ya kukosa maji kabisa tofauti na hivyo vijiji vingine vitano ambavyo vilikuwa vinapata maji kwa masaa, hivyo mradi huo ukikamilika utaondoa changamoto ya maji ya muda mrefu vijiji vya Elerai na Gitu.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Mhandisi Alex Odena alisema, Mradi wa Maji Kwamaligwa- Gitu unatekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Maji (NWF) na kusimamiwa na RUWASA, ambapo chanzo cha maji cha mradi huo ni Bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 670,902,360 kwa mwaka, ambapo mahitaji ya watu kwa siku ni lita 906,575 sawa na lita 330,899,875 kwa mwaka.

Mhandisi Odena alisema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi MS NIPO AFRICA ENGINEERING CO. LTD, ambapo muda wa utekelezaji wake ni miezi 12 na utahudumia jumla ya watu 36,263 ambapo kati ya hawa Kata ya Kibirashi watu 32,641 na Kata ya Kisangasa Kijiji cha Kwediswati watu 3,622.
“Ujenzi wa mradi huu ulianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, Machi 7, 2024 na kutarajiwa kukamilika Aprili 6, 2025, lakini kutokana na sababu mbalimbali, mradi huu sasa unatarajiwa kukamilika Septemba Mosi, 2025. Utekelezaji wa mradi huu kwa ujumla umefikia asilimia 50, ukihusisha ujenzi wa kidakio (Intake) asilimia 50, ujenzi wa kibanda cha mitambo asilimia 70. na ujenzi njia ya umeme asilimia 60.
“Ujenzi wa matenki ya maji yenye mita za ujazo 1,000 (lita milioni moja) na 300 (lita 300,000) asilimia 50, ununuzi wa bomba, uchimbaji mtaro,ulazaji na uunganishaji bomba umbali wa mita 49,265 asilimia 60, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 47 asilimia 20, wakati ununuzi na ufungaji wa pampu ya kusukuma maji, ujenzi wa ofisi ya usimamizi wa mradi-CBWSO’s na ujenzi wa uzio kuzunguka kibanda cha mitambo na tanki za maji bado kuanza” alisema Mhandisi

Mhandisi Odena alisema mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu sh. 6,988,881,532, ambapo mpaka sasa Mkandarasi ameshalipwa sh. 1,566,595,450. Mradi huo utakapokamilika utawezesha wananchi wapatao 36,263 wa vijiji sita vya Kata ya Kibirashi na kijiji kimoja Kata ya Kisangasa kunufaika na huduma ya maji safi na salama, hivyo kuwa na ongezeko la asilimia 9.7 la wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo.
“Tunaishukuru Serikali ya
Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayolenga kuboresha miundombinu ya maji kwa wananchi wa Tanzania”amesema Mhandisi Odena.



More Stories
Balozi Nchimbi aongoza waombolezaji kumuaga Mzee Mongella
Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mama yake mzazi
Sheikh Kabeke asisitiza maadili na amani kuelekea uchaguzi 2025