December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JNHPP kuwa Injini ya ukuaji uchumi wa Tanzania

Na Penina Malundo,TimesMajira Online

WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) utakapokamilika unakuwa injini itakayochochea ukuaji wa shughuli za kimaendeleo na uchumi wa Taifa kwa kasi kubwa.

Dkt. Kalemani ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika mradi huo wa JNHPP, ambapo umeme utakaozalisha utakuwa wa bei nafuu wa jumla ya megawati 2115.

Amesema, umeme huo utatumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo na hivyo kuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

“Utekelezaji wa Mradi huu Mkubwa na wa kimkakati ulianza Mwezi Juni 2019 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2022. Lengo la Serikali ni kuhakikisha mradi wa Julius Nyerere unakamilika ndani ya wakati” Amesema Dkt. Kalemani

Aidha, Waziri Kalemani amesema kuwa kulingana na mpango kazi uliopo, Serikali ya Tanzania imeshamlipa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo zaidi shilingi trilioni 1.49 ambayo ni sawa na asilimia 22 ya malipo yote mpaka kukamilika kwa Mradi.

Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2020/21, Serikali tayari imetenga kiasi cha Shilingi za Tanzania Trilioni 1.44 kwaajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali za Mradi wa huo wa JNHPP.

Kwa mujibu wa Dkt. Kalemani, mradi wa JNHPP utakuwa ni kama injini ya uchumi wa Tanzania, kwani kukamilika kwake kunatarajiwa kushusha bei ya umeme na kukuza uwekezaji hasa sekta ya viwanda nchini itakayozalisha ajira pamoja na kuongeza vipato vya wananchi pamoja na pato la Taifa.

Mradi wa Julius Nyerere unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani ambazo ni kiasi cha shilingi trilioni 6.558 mpaka kukamilika kwake.

Mradi huu pia, utasaidia kuhifadhi mazingira na kupunguza ukataji wa miti kutokana na kushuka kwa gharama za umeme.

Ameongeza kuwa, mradi wa JNHPP ndio utakao tatua matatizo ya umeme nchini hivyo kukamilika kwake kuna tija kubwa sana kwa Taifa na Mwananchi mmoja mmoja kwa ujumla.