Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari ameshiriki katika ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama inayoendelea katika Mikoa ya Rukwa na Katavi huku akiipongeza tume hiyo kwa hatua zilizofikiwa na Mahakama katika kuboresha miundo mbinu yake na kurahisisha utendaji kazi wa Mahakama.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa mujibu wa Ibara ya 112 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika ziara hiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameongozana na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ambapo aliongoza kikao hicho huku akimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa kiungo muhimu baina ya Serikali na Mahakama katika masuala mbalimbali ikiwemo Utungaji wa Sheria ambazo zimerahisisha utendaji kazi katika Mahakama.
“Tunamshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutengeneza na kuboresha sheria mbalimbali ambazo zimerahisisha utendaji wa haki kwa urahisi na kupunguza mlundikano wa mashauri,”amesema Prof. Juma
Aidha, Jaji Mkuu alimpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za maboresho ya Mahakama na kuipa kipaumbele ziara hiyo ya Tume ya Utumishi wa Mahakama licha ya kuwa na ratiba ngumu zinazomkabili.

“Tunakupongeza Mh. Johari kwa ushiriki wako katika masuala mbalimbali yanayoihusu Mahakama pamoja na kuipa umuhimu ziara hii pamoja na kukabiliwa na ratiba ngumu ikiwemo vikao vya Bunge linaloendelea”,amesema Jaji Mkuu.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Johari amesema amefurahishwa na hatua zilizofikiwa na Mahakama katika kuboresha miundo mbinu yake hivyo kurahisisha utendaji kazi wa Mahakama.

“Niipongeze sana Tume ya Mahakama kwa kuboresha miundombinu ya mahakama katika mikoa mbalimbali nchini hivyo kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi,”amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu huyo amehudhuria kikao cha Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Watumishi wa Mahakama wa Mkoa wa Katavi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
More Stories
NEC yachagua wajumbe wa kamati kuu,yumo Asas
Waziri Aweso atoa maelekezo kwa Wakurugenzi huduma za maji nchini
Serikali yataka kuongezwa kwa vituo vya TEHAMA