May 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mkenda:Elimu ya biashara somo la lazima kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof.Adolf Mkenda amesema kuwa kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 iliyozinduliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,Februari Mosi mwaka huu mabadiliko mengi na makubwa yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza muda wa elimu ya lazima kuwa miaka 10.

Muundo katika mfumo rasmi wa elimu na mafunzo kuwa 1+6+4+2/3+3+, pamoja na kuweka Mfumo wa elimu unaozingatia kuandaa wahitimu wenye ujuzi kwa kuanzisha mkondo wa amali kuanzia sekondari.

Amesema Sambamba na Sera hiyo wamefanya mabadiliko na maboresho katika mitaala ya elimu Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu. Mabadiliko makubwa ni pamoja na kuweka mikondo miwili ya Elimu ya Sekondari Mkondo wa Jumla na Mkondo wa Amali na kuweka mfumo wa elimu kuwa nyumbufu.

Ambapo katika mitaala hiyo wameanzisha somo la lazima kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne la elimu ya Biashara na Historia ya Tanzania pamoja na kuimarisha mifumo ya ufundishaji lugha.

Prof.Mkenda amesema hayo jijini hapa leo Mei,27,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Hali kadhalika upande wa elimu ya ufundi mitaala 389 na elimu ya juu Mitaala 563 imenzishwa na kuboreshwa ili iendane na Sera na kuzingatia stadi za karne ya ishirini na mahitaji ya kiujuzi kitaifa kikanda na kimataifa. Msemo mkubwa sasa katika jamii ni Elimu na ujuzi ndio mpango mzima,”amesema Prof.Mkenda.

Aidha amesema kuwa Katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sera na mitaala iliyoboreshwa, Serikali imeanza mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ili kuendana na matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 ambapo maoni ya wadau mbalimbali wa elimu kuhusu sheria husika yameendelea kukusanywa.

“Serikali imeendelea kuhuisha na kuandaa miongozo mbalimbali ya utoaji elimu na mafunzo nchini ili kuendana na matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023,”amesema

Vilevile amesema Katika kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi, wizara imeanzisha Mikopo kwa wanafunzi wa stashahada kwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 19.95 kwa wanafunzi 7,534 wa fani za sayansi na ufundi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa ni ongezeko la asilimia 177.6 ikilinganishwa na wanafunzi 2,714 wa mwaka wa fedha 2023/24.

Pia amesema Rais alizamia kuongeza idadi ya wanafunzi katika masomo ya Sayansi hivyo wakaanzisha Samia Scholarship kwa wanafunzi waliofaulu vizuri masomo ya Sayansi kidato cha sita na kujiunga katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Elimu Tiba na Hisabati.

“Serikali imeendelea kutoa ufadhili wenye thamani ya shilingi bilioni 18.7 kwa wanafunzi 674 wa mwaka wa kwanza na 669 wanaoendelea wenye ufaulu uliojipambanua katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati kupitia SAMIA Skolashipu. Kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Samia Scholarship Extended inafadhili shahada za juu ikiwemo eneo la sayansi na teknolojia ya nyuklia,”amesema Prof.Mkenda