May 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali inavyoimarisha mifumo ya kisheria nchini

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum imeendeleza mikakati madhubuti ya kuimarisha mifumo ya kisheria, kijamii na kielimu.

Hayo yamesema leo Mei 27,2025 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Dorothy Gwajima wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2025/2026 ambayo imeomba kiasi cha shilingi bilioni 76.05 ili iweze kutekeleza majukumu yake  katika kipindi hicho.

Amesema hatua hizo zimejikita kwenye kuondoa mianya ya kisheria, kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali na kufanya kampeni za kitaifa zenye mguso wa moja kwa moja kwa watoto, wazazi na walezi.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, Wizara ilifanya marekebisho ya Sheria ya Mtoto (Sura ya 13), Sheria ya Makosa ya Kimtandao (Sura ya 443) na Sheria ya Msaada wa Kisheria (Sura ya 21) kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili na unyanyasaji, hususan kwenye mazingira ya kidigitali ambayo yameendelea kuwa tishio jipya kwa watoto.

Aidha amesema, Serikali iliratibu mafunzo ya kitaalamu kuhusu Sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa Maafisa 281 kote nchini.

“Mafunzo haya yaliwalenga maafisa kutoka mikoa na halmashauri ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi (MMMAM 2021/22–2025/26).”amesema na kuonhgeza kuwa

“ Katika hatua ya kipekee, waandishi wa habari 26 kutoka kila mkoa walipewa mafunzo hayo ili wawe mabalozi wa kutoa elimu hiyo kwa jamii kupitia vyombo vya habari.”

Vile vile amesema,kupitia Kampeni ya Taifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni (COP), Serikali ilifika moja kwa moja kwa wazazi/walezi zaidi ya 821,098 na wanafunzi 786,901 katika shule za msingi na sekondari.

Amesema,mafunzo haya yalikusudia kumjengea mtoto uwezo wa kutumia mitandao kwa usalama na kuepuka hatari za udhalilishaji wa kidijitali.

“ Ili kuongeza ufanisi, Wizara iliunda Kamati ya Taifa ya Ushauri ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni yenye jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu mikakati ya ulinzi wa mtoto katika nyanja hiyo.”

Dkt.Gwajima amesema,juhudi hizo zinasindikizwa na matokeo ya wazi ambapo katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, matukio ya ubakaji yamepungua kwa asilimia 6.3, kutoka 8,185 hadi 7,670.

Aidha amesema, matukio ya ulawiti yakipungua kwa asilimia 19 kutoka 2,382 hadi 1,930 huku akisema hiyo ni  ishara ya ushahidi kwamba sera na afua zinazotekelezwa na Serikali zina tija.

“Kwa ujumla, hatua hizi za kitaifa zinaonesha kuwa haki na maendeleo ya mtoto si suala la hiari bali ni ajenda ya kipaumbele katika ujenzi wa Taifa lenye usawa, usalama na matumaini kwa vizazi vijavyo.”amesisitiza Waziri huyo