May 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yafanya tukio la utayari wa majanga ya moto

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

KUTOKANA na changamoto ya matukio ya moto yanayoendelea katika maeneo mbalimbali  hapa nchini Benki ya NMB imeandaa zoezi la utayari ili kujiandaa na kujikinga na  majanga ya moto.

Akizungumzia tukio hilo Mei 26,2025 Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Mwanjelwa ,Lembrus Israel amesema kuwa tukio la moto linaweza kutokea sehemu yeyote katika jamii hivyo ni muhimu kujiweka  na utayari katika kukabiliana nayo .

“Leo tumepata tukio ambalo linaweza kutokea mahali popote ikiwemo kwenye familia, Taasisi,mali, biashara, mashamba, moto unaweza ukatokea ni majanga ambayo hawakutegemea lakini leo wamekubwa na janga la moto, majanga haya hayatabiliki na hayazuiliki lakini tulivyopata janga hili tuliweza kuwapigia wenzetu wa jeshi la zimamoto, polisi, hospitali ya rufaa  kanda ya Mbeya,Tanesco ili waweze kuja kukata umeme katika jengo hili “amesema Israel.

Aidha Meneja huyo ameshukuru majeshi yote kwa kuweza kufika  kwa wakati na kuweza kuthibiti moto na kuwa moto huo umeweza kuthibitiwa kwa asilimia 99.

Akielezea zaidi Israel amesema majanga ya moto hayatabiriki na kuwa benki ya NMB inatoa bima za majanga kama hayo ikiwemo Moto,vifo na kuunguliwa na mali zao hivyo  kuwataka wateja wote kukata bima ili waweze kufidiwa na kuwa majanga yanapotokea mali  zote huteketea.

Hata hivyo  Meneja huyo ameeleza kwa kupitia bima za Benki ya NMB ambazo Taasisi hiyo inatoa inahimiza wananchi wa mkoa wa Mbeya  kutumia Benki hiyo kukata bima ambazo zitawafidia pindi wanapokutwa na majanga ya moto.

“Lakini tukio hili leo Mei 26,2025 tuliweza kupata tukio hili ilikuwa zoezi la kujiweka utayari kwa majanga ya moto ambayo yanatokea  na katika kujikinga na majanga haya  ya moto pamoja uko utimamu basi tukasema tufanye tukio hili la utayari wa moto wa kujikinga “amesema Meneja huyo.

Aidha amesema kuwa yale yaliyotokea hakuna madhara yaliyotokea  wale majeruhi wamepelekwa hospitali  Kitengo cha dharura na kupokolewa vizuri kwa yale waliyokuwa wanategemea na kushukuru polisi na  jeshi la zima moto kwa ushirikiano mkubwa.

“Tukio hili nilikanushe lilikuwa tukio la kujiweka utayari na majanga ya moto ,na fedha zenu wateja zipo salama kabisaaa ndugu zangu niwatoe hofu katika hili”amesema.

Kwa upande wake mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya (OCD)Magnus Milinga amewataka wananchi pale matukio ya moto yanapotokea wawe na utulivu na fedha na mali zote zipo salama, zoezi hilo lilikuwa la utayari na limeshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa upande wake Ofisa Oparesheni wa Jeshi la Zima Moto mkoa wa Mbeya,Gervas Fungamali amesema kuwa tukio hilo ni kama linakuwa na uhalisia na kuwa ndani kulikuwa na wafanyakazi wawili ambao waliokolewa na kufikishwa hospitali.

“Nitoe wito kwa wananchi mpatapo  tukio kama hili leo hii ni Benki ya NMB lakini kesho unaona soko linaungua na hata nyumbani kwako basi piga namba ya dharura ambayo nj 114 ,namba hii ni bure Sasa changamoto ambayo huwa inatokea wananchi wengi wanaanza kujisaidia kuzima moto na kusahau kuwa wanatakiwa kujulisha jeshi la zima moto,hivyo na sisi tushukuru Benki ya NMB kwa mazoezi kama haya kwani yanatuweka tayari na kama jeshi to najipima kwa Matukio haya “amesema.