Na Penina Malundo, Timesmajira
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda ameeleza kuwa kituo cha umahiri cha Afrika Mashariki cha Sayansi ya Moyo na Mishipa ya Damu kitanufaisha nchi za jumuiya hiyo, haswa katika Nyanja za matibabu ya kibingwa.
Profesa Mkenda ameyasema hayo jana Ijumaa, Mei 23, 2025 alipokuwa akiongoza uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha umahiri chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), Mloganzila jijini Dar es Salaam.

“Hiki ni kituo ambacho kitainufaisha siyo tu Tanzania, bali pia nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hata nchi zilizo nje ya Jumuiya hii zitanufaika pia na kituo hiki cha umahiri,” amesema Profesa Mkenda.

Ameeleza kuwa pamoja na utoaji wa huduma bora za afya kupitia tafiti, mafunzo na tiba, kituo hicho ambacho kinagharimu Dola za Kimarekani milioni 83, takribani Shilingi bilioni 224, kitaongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini kwa ajili ya tiba, maarufu kama ‘medical tourism’.

Uzinduzi wa kituo hicho cha awamu ya pili umekuja kutokana na awamu ya kwanza kukamilika vizuri, ambayo ilijumuisha ujenzi wa jengo la kisasa la kufundisha lenye Maabara, Maktaba, studio za masomo, kituo cha mazoezi, kumbi nane za mihadhara na ukumbi wa mikutano.
More Stories
Suluhu mgawanyo wa mapato wa huduma za usafiri wa anga nchini, wapatikana
Rais Samia awataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi
Madini ya almasi yenye thamami ya Bil.1.7 yakamatwa yakitoroshwa uwanja wa ndege Mwanza