May 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tax:Vyombo vya usalama vinaendelea kuchukua tahadhari ,Taifa lipo salama

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa,limesema Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) Kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Usalama linaendelea kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vyote vyenye viashiria vya Uvunjifu wa  amani na Taifa ni salama na lenye Utulivu na amani.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Mei 22,2025 na Waziri Wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa,Dkt.Stergomena Tax wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema
Wizara kupitia JWTZ,imeendelea kulinda Amani,kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania na kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi ipo salama.

Amefafanua kuwa katika kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,uhuru na Usalama wa nchi,JWTZ imechangia Katika Uchumi imara kwa wananchi kuendelea na Shughuli za kuzalisha mali bila hofu na wananchi kutumia muda wao mwingi kujenga Uchumi wa Nchi.

Hata hivyo,amesema Serikali kupitia Wizara hiyo inaendelea kuliimarisha Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kwa kuliongezea Bajeti,na hivyo kuongeza uwezo wa kimedani Kwa kulipatia vifaa,zana za kisasa na kuwezesha mafunzo na mazoezi.

Aidha Dkt.Tax amesema kuwa amesema kuimarika Kwa jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania,kumechangia Nchi kuwa ya Amani na utulivu na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya nchini.

“Serikali ya Awamu ya Sita  imehakikisha tunu muhimu za Taifa yaani amani, ulinzi na usalama zinalindwa kwa kuimarisha umoja, mshikamano na utulivu nchini,”amesema.

Pamoja na hayo Dkt.Tax amesema Wizara kupitia SUMAJKT imefanikiwa kuchangia katika ujenzi wa uchumi ili kuipunguzia Serikali gharama za uendeshaji wa mafunzo kwa vijana wa JKT kwa kutekeleza miradi ikiwemo ya ujenzi wa vituo vya madini katika baadhi ya mikoa, baadhi ya majengo ya Halmashauri za Wilaya na majengo ya Taasisi za Serikali.

“SUMAJKT imeimarisha viwanda vyake ikiwemo,kiwanda cha Maji ya kunywa Mgulani kilichofikia uwezo wa kuzalisha katoni 2500 za nusu lita na 4400 za lita moja kwa siku na kiwanda cha ushonaji Mgulani chenye uwezo wa kuzalisha mavazi ya kijeshi 300 hadi 400 kwa siku.

“Viwanda vingine ni kiwanda cha bidhaa za ngozi Mlalakuwa, kiwanda cha Kuchakata mahindi Mlale Songea chenye uwezo wa kuchakata tani 20 kwa siku, Kiwanda cha Samani Chang’ombe na kiwanda cha taa za LED kilichopo Dar es Salaam,”amesema.

Vilevile SUMAJKT imechangia jumla ya shilingi 2,667,084,941.00 kwa ajili ya kugharamia shughuli za malezi ya vijana wa JKT na imetoa gawio kwa serikali jumla ya shilingi 4,275,050,000.00.

Pia Katika utekelezaji wa mkakati wa kilimo, jumla ya kiasi cha tani 9165.3 za mahindi, tani 2,883.4 za mpunga, tani 144.1 za Alizeti na tani 44.4 za maharage zimezalishwa ambapo kati yake, tani 5,034 za mahindi, tani 2883.4 za mpunga, tani 144.1 za Alizeti na tani 44.4 za maharage zimetumika kulisha vijana wanaohudhuria mafunzo ya JKT na tani 2588.9 za mahindi zimechangia katika usalama wa chakula.