May 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mixx by Yas, UBX, SCCULT kushirikiana kurahisisha huduma za mikopo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MIXX by Yas imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Kampuni ya UBX na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), kama mshirika rasmi wa malipo kidijitali kwa wanachama wa chama hicho Tanzania nzima.

Kupitia ushirikiano huo, wanachama wa SACCOs wataweza kuweka akiba na kufanya marejesho ya mikopo kwa njia rahisi na salama kwa kutumia Mixx by Yas, bila kujali mtandao wa simu wanaotumia.

Mfumo huo mpya unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa kwa Watanzania waliopo maeneo ya pembezoni.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha (kulia) na Seronga Wangwe, Afisa Mkuu Mtendaji wa UBX (kushoto) wakibadilishana vyeti vilivyosainiwa kufuatia makubaliano ya kimkakati kati ya Mixx by Yas, UBX, na Umoja wa Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT). Katika hafla fupi iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia tukio hilo ni Dkt. Khadija Kishimba, mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Dkt. Khadija Kishimba mwakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania, akimuwakilisha Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kennedy Komba amesema ni hatua kubwa katika kujenga mfumo jumuishi wa kifedha kwa Watanzania wote.

“SACCOs zina mchango mkubwa katika kuwafikia wananchi walioko maeneo yenye changamoto za upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha.

“Ushirikiano kati ya Mixx by Yas na UBX ni mfano bora wa jinsi sekta binafsi inavyoweza kusaidia kufanikisha ajenda ya kitaifa ya ujumuishaji wa kifedha,” amesema Kishimba.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha amesema ushirikiano huu unalenga kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa wanachama wa SACCOs kwa kutumia teknolojia ya simu za mkononi.

Kupitia suluhisho hilo la kidigitali, wanachama wa SACCOs wataweza kuweka akiba, kurejesha mikopo na kupata huduma nyingine za kifedha bila kutembelea ofisi wala kujaza makaratasi.

“Mixx tunaamini kuwa kila Mtanzania, popote alipo, anapaswa kupata huduma za kifedha kwa njia rahisi, salama na ya kisasa.

“Ushirikiano huu ni hatua ya mabadiliko, hasa ikizingatiwa kuwa chini ya asilimia 5 ya SACCOs ndizo zinazotumia teknolojia ya simu za mkononi kutoa huduma leo hii,” amesema Pesha.

Takwimu za Ripoti ya Finscope ya mwaka 2023 zinaonyesha kuwa ni asilimia 2 tu ya Watanzania ndio wanaotumia huduma za SACCOs, licha ya mchango wake mkubwa kwa jamii za mijini na vijijini.

Ushirikiano huo wa Mixx, UBX na SCCULT unalenga kubadili hali hiyo na kuwezesha wanachama wa SACCOs kupata huduma kwa urahisi kupitia simu zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UBX, Seronga Wangwe amesema kupitia mfumo huoSACCOs zitakuwa na uwezo wa kutoa mikopo papo kwa papo huku zikihakikisha uwazi na usahihi wa takwimu.

“Hii ni hatua muhimu katika kujenga uaminifu baina ya SACCOs na wanachama wao. Mfumo huu mpya, unatarajiwa kuanza kutumika rasmi katika robo ya tatu ya mwaka 2025 kwa SACCOs zote zilizo chini ya SCCULT,” amesema Seronga.

Lengo kuu la ushirikiano huo ni kupunguza ucheleweshaji wa huduma, makosa ya kibinadamu, utegemezi wa makaratasi, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kifedha vijijini na mijini.