May 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwongozo wa kitaifa kwa watoa huduma za maendeleo ya biashara wazinduliwa

Na Mwandishi wetu,Timesmajira Online 

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt.James Kilabuko amezindua rasmi mwongozo wa kitaifa kwa watoa huduma za maendeleo ya biashara ambao umelega kuboresha utoaji wa huduma hizo .

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Mei 21, 2025, kwa Niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, Dkt Kilabuko amesema kuwa mwongozo huo unaweka msingi wa mabadiliko, ambayo yatawawezesha wafanyabiashara wadogo,wa kati na wafanyabiashara wakubwa kukuza biashara zao na kuchangia kikamilifu kwenye uchumi wa taifa.

“Uwepo wa Mwongozo huo unalenga kuweka viwango, mwelekeo na uratibu wa huduma zinazotolewa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini, umekuja kwa wakati sahihi na tunaamini utaleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa,” amesema Dkt. Kilabuko na kuongeza:

“Rais  ameboresha mazingira ya biashara nchini na kuchochea kuanzishwa kwa shughuli za kiuchumi nyingi katika sekta mbalimbali. Shughuli hizo pia zinahitaji huduma za maendeleo ya biashara ili kuwa shindani,”.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Beng’i Issa,amesema kuwa mwongozo huo unalenga kuboresha utoaji wa huduma za biashara ikiwemo ushauri, mafunzo, msaada wa kiufundi, ujuzi, uatamizi, uhusiano baina ya wafanyabiashara, mawasiliano na usimamizi wa biashara.

“Tunategemea,mwongozo huu unakwenda kutoa dira ya namna bora ya utoaji wa huduma za biashara Tanzania, zinazoweza kuboresha biashara na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema Beng’i.

Hivyo amewasihi watoa huduma za maendeleo ya biashara nchini kutumia mwongozo huo kama nyenzo katika kuwahudumia wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaotekeleza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali. 

Naye Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano na wanathamini uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yao na Tanzania,hivyo wataendelea kushiriki katika masuala mbalimbali ikiwemo kuunga mkono sekta ya afya, elimu, biashara, uwekezaji, kilimo, ulinzi na usalama. 

Mkurugenzi Mkazi wa MEDA,Musa Lugambo amesema kuwa mwongozo huo utawasaidia watoa huduma kutoa huduma ambayo itawasaidia wajasiriamali kwa ajili ya kutekeleza biashara zao. 

“Tumekuwa na changamoto kwa watoa huduma,unakuta kwamba huduma ambayo inayotolewa kwa wajawasiriamali inakuwa siyo ya kiwango kizuri na hivyo kushindwa kuwasaidia wajawasiriamali kuendeleza biashara zao,”amesema Lugambo.