May 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Lulida :Mjusi wa Tendaguru,’Mapato yetu yanaliwa Ujerumani, Lindi Inabaki Maskini

Na Joyce Kasiki – TimesMajira Online, Dodoma

MBUNGE wa Kuteuliwa, Riziki Lulida  ameikosoa vikali Serikali kwa kushindwa kufuatilia mapato yanayotokana na mabaki ya mjusi wa kihistoria  aliyegunduliwa eneo la Tendaguru, mkoani Lindi, na kupelekwa Ujerumani.

 Amedai kuwa, licha ya mjusi huyo kutumika kibiashara na Wajerumani kwa miongo kadhaa, Tanzania haijanufaika kwa kiwango chochote, huku vijiji alikotoka mjusi huyo vikikosa maendeleo ya msingi.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Mei 19, Mhe. Lulida alisema:

“Mimi ni Balozi wa Utalii, cheo nilichopewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Lakini sitakuwa na furaha katika nafasi hiyo kama mjusi wa nchi yangu hauniletei faida yoyote. Hatutakubali kukaa kimya juu ya suala la mjusi. Huu ni urithi wetu wa kitaifa.”

Mhe. Lulida alieleza kuwa tangu mwaka 2007 amekuwa akifuatilia suala hilo bungeni, lakini Serikali haijachukua hatua madhubuti kuhakikisha nchi inanufaika na mapato yanayotokana na maonesho na matangazo ya biashara yanayomhusu mjusi huyo nchini Ujerumani.

“Wenzetu wa Namibia walidai na kupata mapato kutoka kwa wageni waliobeba urithi wao. Sisi Tanzania tunashindwa nini? Hakuna msaada wowote tuliopata kutoka kwa Wajerumani, na bado wanatumia mjusi huyo kwenye sinema kubwa na matangazo ya kimataifa, huku vijiji vya Namapwia, Mipingo, Matapwa, Makangaga na Namnyangara vikibaki nyuma kimaendeleo,” alilalamika kwa uchungu.

Mbunge huyo pia alieleza kuwa lengo lake si kuurejesha mjusi huyo nchini bali kuhakikisha kuwa mapato yote yaliyotokana na mjusi huyo yanagawanywa kwa haki. Alisisitiza kuwa Serikali inapaswa kudai tozo za miaka yote ambazo Wajerumani wamekuwa wakinufaika kupitia mjusi huyo.

“Tunataka mkoa wa Lindi, halmashauri yake na vijiji husika vinufaike. Hii ni pamoja na kupata huduma za kijamii kama shule, zahanati, barabara na maji kutokana na mapato ya mjusi wetu,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Lulida alipinga vikali kuundwa kwa kamati ya kushughulikia suala la mjusi bila yeye kuhusishwa. Alidai kuwa kamati hiyo haina uhalali wowote kwa kuwa yeye ndiye amekuwa mstari wa mbele kutetea mjusi huyo tangu mwaka 2005.

“Haiwezekani kuunda kamati ya mjusi bila kuhusisha Balozi wa Utalii ambaye amekuwa mstari wa mbele kwa miaka mingi. Nilipowauliza watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kama wanapafahamu alikotoka mjusi hawakuwa na jibu. Mimi ndiye nimekuwa nikiwafumbua macho. Kamati hiyo ni batili,” alisisitiza.

Mwisho, alitoa wito kwa Serikali na wabunge kuhakikisha suala la urithi wa kihistoria kama mjusi wa Tendaguru linapewa uzito wa kipekee, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.