Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Mpwapwa
IBADA ya maombezi ya nchi ya Tanzania na viongozi wake wa serikali ya awamu ya sita imefanyika katika kijiji cha Pwaga Jimbo la kibakwe wilayani Mpwapwa katika kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba mwaka huu.
Katika idaba hiyo iliyoongozwa na viongozi wa dini kutoka madhebu mbalimbali wamesema lengo la ibada hiyo ni kuiombea Nchi pamoja na viongozi wake wakiongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,Kwa kuiombea Nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa nafasi za Rais,Wabunge na Madiwani ili kuweza kupata Viongozi bora kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ambao watasimamia kuleta maendeleo kwa Nchi na wananchi wake.
Viongozi hao wamesema kuwa Hayati baba wa Taifa Mwalimu Juliasi Nyerere alileta umoja na mshikamano mkubwa kwa makabila yote na ndiyo maana mtanzania yoyote anaishi sehemu yoyote ile bila kuulizwa wewe kabila gani hivyo jambo la amani na utulivu siyo la kulichezea kabisa.
Naye Diwani wa kata ya Pwaga, Wille Mgonela amewasisitiza wananchi wa kata ya Pwaga kuhakikisha wanaendelea kuilinda amani na huku akiwadisitiza wananchi kujitokeza kwenye zoezi linaloendelea sasa la Kujiakisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kidumu la mpiga kura ili kila mwananchi mwenye Umri kuanzia miaka 18 ahakikishe anatumia fursa hiyo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mpwapwa Comredi Saidy Mguto amesema kuwa wao kama chama wanashukuru Serikali kupitia tume huru ya uchaguzi kwa kuwaletea daftari la kujiandikisha kwa awamu ya pili sasa ili kila mwanachama na mwananchi apate kutumia fursa hiyo kuhakikisha anajiandikisha.
“Kwa sisi wana siasa tunasema mtaji wetu wa wapiga kura halali unatokana na wanachama na wananchi kujiandikisha katika hili daftari la mpiga kura na ndiyo maana sisi tumehakikisha wanachama wetu wote wamepatiwa elimu juu ya umuhimu wa kujiandikisha au kuboresha taarifa zao kwenye daftari hili Muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba mwaka huu”amesisiza Comredi Mguto.
Mgeni Rasmi katika ibada hiyo ya maombi Mbunge wa Jimbo la kibakwe na Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,George Simbachawene amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la kibakwe imetekeleza Ilani ya chama cha Mapinduzi kwa asilimia kubwa kwa kupeleka fedha za maendeleo katika sekta mbalimbali katika kata zote za Jimbo ambalo analiongoza.
Aidha Simbachawene amebainisha baadhi ya maendeleo katika sekta ya afya ikiwemo Ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya katika kata za Ipera,Rudi,Mtera,kibakwe,Pwaga,chipogolo,wotta .
Simbachawene amesema kuwa pamoja na muendelezo wa ujenzi wa vituo vya Afya Kata ya Mbuga,Mlunduzi ambao Ujenzi wake unaelekea kuanza muda siyo mrefu kwakuwa fedha za Ujenzi wa vituo hivyo tayari zimeshapatikana kwa kuanza kazi.
Kwa upande wa Elimu Waziri Simbachawene amesema kuwa tayari wameboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kwa walimu na wanafunzi ujenzi wa nyumba za walimu,vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo pamoja na kuzipandisha hadhi baadhi ya shule za sekondari kuwa za Kidato cha tano na sita ikiwepo Shule ya Sekondari Mtera.
Pia Simbachawene amesema katika shule za Sekondari za kata wameziboresha zaidi kuwa za kisasa Zaidi na kuwa walau na walimu wa kutosha kutokana na masomo yanayo fundishwa shuleni hapo.
Aidha Waziri Simbachawene amesema katika suala la nishati ya umeme katika Jimbo lake umeme umewafikia wananchi wote wa kata 18 zilizopo jimbo la kibakwe na kuwanufaisha wananchi wengi katika kujikwamua kiuchumi kupita nishati ya umeme.
Waziri simbachawene amesema suala la miundombinu limeboreshwa kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwani maeneo ambayo miaka kadhaa iliyopita yalikuwa hayapitiki kwa Sasa TARURA walishapasua hivyo katika jimbo la Kibakwe sehemu zote zinafikika kwa gari japo bado kunachangamoto kipindi cha mvua baadhi ya maeneo lakini TARURA wameshayapitia maeneo yote hivyo yatapata tiba yake kupitia mwaka wa fedha ujao kwani bajeti imeshatengwa.
Simbachawene pia amewashukuru viongozi wa Dini kwa maombezi ya kuiombea Taifa na amewashukuru wananchi wa Jimbo la kibakwe kwa kujitokeza kubuni miradi malimbali ya maendeleo na amewasisitiza kuhakikisha wanajitokeza kujiandikisha kwenye daftari hilo Muhimu na kuboresha taarifa zao ili ifikapo Oktoba mwaka huu waweze kuwachagua viongozi ambao watawaketea maendeleo kuanzia Rais, wabunge na madiwani.



More Stories
Kamishina TRA avitaka Viwanda viwili Mkuranga kulipa kodi inayostahili
Naibu Meya Masaburi apewa uanachama wa heshima umoja wa LITONGO
Wanafunzi Ilala Boma wafanya ziara ya Masomo uwanja wa ndege